Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema utekelezaji wa miradi upande wa Zanzibar ni matunda ya ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Amesema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini wa makabidhiano ya eneo la mradi kwa ufukwe wa Sipwese, Pemba kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi ambapo mradi huo utatekelezwa na Kampuni ya Dezo Civil Contractors Co. Limited.
Mhe. Hemed alisema kuwa SMZ inafarijika kuona mradi huo unaanza kutekelezwa kwa vitendo na kwamba utaleta manufaa makubwa kwa wananchi watakaonufaika na mradi huo.
Pia alitumia nafasi hiyo kutoa pongeza na shukrani kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango pamoja na Ofisi yake kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa SMZ.
Awali akitoa taarifa kuhusu mradi huo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Bi. Mary Maganga, alisema tathmini katika ufukwe wa Sipwese ilionesha kuwa maji ya bahari yameingia katika maeneo ya kilimo cha mpunga na wananchi wa Shehia ya Mkungu, Kijiji cha Sipwese eneo la kwa Mgogo.
Mitawi alisema kujaa kwa maji haya pia yamesababisha kukatika kwa mawasiliano kutoka upande wa pili takribani kilometa 3.360 ambako ndiko wananchi wanafuata huduma za jamii kama vile shule hali inayosababisha watoto wa shule kuvuka maji shingoni kuweza kuifikia shule.
“Mmomonyoko wa fukwe zilizo katika Bahari ya Hindi kwa upande wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani umeendelea kuwa ni changamoto katika maeneo mengi ya fukwe na umeanza kuleta athari katika baadhi ya maeneo kwa kusababisha uharibifu wa miundombinu iliyopo kama vile barabara, majengo, makazi ya watu na madaraja.
“Hali hii imesababisha Serikali kutumia fedha nyingi katika kukarabati miundombinu iliyoharibiwa, Fedha ambayo ingeweza kupelekwa katika maeneo mengine muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijami,” alisema Mitawi.