Makamu wa Pili wa Rais aipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutoa Elimu ya Muungano

Apr, 19 2024

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutoa elimu kuhusu masuala ya Muungano.

Ametoa pongezi hizo wakati akizindua maonesho ya Biashara ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar- es- Salaam ikiwa ni katika shamra shamra za sherehe za miaka 60 ya Muungano.

Amesema kuwa banda la maonesho la Ofisi ya Makamu wa Rais lililopo katika viwanja hivyo limesheheni vitabu na maandiko mbalimbali yanayohusu Muungano adhimu.

Mhe. Hemed ambaye alitembelea banda hilo mara alipowasili, ametoa wito kwa wananchi wote kulitembea na kupata elimu kutoka kwa wataalamu wa Ofisi hiyo.

Aidha, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itaendelea kuuenzi kuulinda Muungano huku akiwataka wananchi kushiriki katika kuujua Muungano.

Halikadhalika, Makamu wa Pili wa Rais amesema kuwa uwepo wa Muungano umechangia kuimarika kwa huduma za kijamii kwa pande zote mbili za Muungano kama vile Sekta ya Maji safi na salama, Afya, elimu, ustawi na maendeleo ya jamii, makazi na usafiri.

Amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa udugu wa damu na urafiki ambao umepunguza migawanyiko ya kijamii na kuondoa hisia za ukabila na ubaguzi miongoni mwa wananchi.

Mhe. Hemed ameeleza kuwa ustawi wa wananchi umeimarika na kukua kwa uchumi kulikotoa fursa kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo kuwekeza katika pande zote mbili za Muungano katika sekta ya Viwanda, Hoteli na kilimo cha biashara jambo ambalo linachangia kuongeza ajira kwa wananchi.

Settings