Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman ameishauri Ofisi ya Makamu wa Rais kushirikiana na Ofisi yake katika kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi Zanzibar.
Amesema hayo alipokutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji aliyefika ofisini kwake kujitambulisha baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, wakati wa ziara yake Zanzibar.
Mhe. Othman amesema kuwa Zanzibar hususan Pemba imekuwa ikiathiriwa kwa kiwango kikubwa na maji ya chumvi kuingia katika makazi na mashamba ya kilimo na hivyo kuathiri mustakbali mzima wa maisha ya kila siku.
Amezitaka taasisi mbili za mazingira ambazo ni Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Baraza la Mazingira (ZEMA) kukaa na kutafakari kwa pamoja mbinu na hatua za kuchukua.
Awali Mhe. Dkt. Kijaji wakati alipofanya ziara katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais aliahidi kutenga siku zake za kazi katika kila mwezi kukaa na kufanya kazi zake katika ofisi yake ya Zanzibar lengo ikiwa ni kurahisisha utendaji wa majukumu yake.
Wakati akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wakilishi) Hamza Hassan Juma pamoja na mambo mengine walikubaliana kuimarisha mashirikiano katika utendaji wao wa kazi.
Halikadhalika, Waziri Mhe. Dkt. Kijaji ameahidi ushirikiano kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ili Serikali zote mbili ziweze kuhudumia Watanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake Waziri Hamza Hassan Juma ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote ya viongozi kutoka pande zote mbili za Muungano yote ni katika kuwahudumia wananchi ili Tanzania isonge mbele.
Hivyo, Mhe. Waziri Juma amemuahidi Mhe. Waziri Dkt. Kijaji ushirikiano na kumkaribisha wakati wowote anapohitaji kubadilishana uzoefu katika kuimarisha Muungano.
Waziri Mhe. Dkt. Kijaji amefanya ziara ya kujitambulisha kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) mara baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.
Wamesema Muungano wa nchi mbili ni wa kindugu na umekua na manufaa kwa pande zote mbili kiuchumi, kijamii na kisiasa.