Majaliwa:Mradi wa bomba la mafuta umezingatia hifadhi ya mazingira

Sep, 23 2022

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga nchini Tanzania umezingatia hifadhi ya mazingira.

Amesisitiza kuwa mradi huo umefanyiwa tathmini ya kina ya kimazingira na kuhakikisha kuwa utekelezaji wake hauna athari zozote za kimazingira na kwa jamii.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo Septemba 23, 2022 wakati akiahirisha mkutano wa Nane wa Bunge la 12 jijini Dodoma na kusema baadhi ya wadau wa maendeleo wamekuwa na mashaka katika utekelezaji wa mradi huo wakihofia kuwa unaweza kutekelezwa pasipo kuzingatia athari za kimazingira na haki za binadamu.

Mhe.Majaliwa alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan inasimamia kikamilifu sekta ya nishati ikiwemo kuendelea kutekeleza mradi huo ili kukuza uchumi.

Alisisitiza mradi huo ni muhimu kwa manufaa ya nchi hizo mbili katika kukuza biashara, viwanda vya uzalishaji, kuongeza ajira pamoja na kuvutia wawekezaji ambao wanatarajia kukuza teknolojia na ujuzi kwa wananchi.

Settings