Dkt. Dugange: NEMC Chukueni sheria kudhibiti uzalishaji kelele

Nov, 28 2025

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuchukua hatua dhidi ya wanaozalisha kelele na mitetemo katika maeneo mbalimbali nchini.

Ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao na Bodi, Menejimenti na watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) alipofanya ziara ya kufuatilia na kujifunza utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo, jijini Dar es Salaam leo Novemba 28, 2025.

Mhe. Dkt. Dugange alisema sheria zinazodhibiti kelele na mitetemo zipo hivyo NEMC wachukue hatua kudhibiti hali hiyo ili kuwanusuru wananchi na changamoto hiyo ambayo huwaletea madhara ya kiafya wananchi.

Alibainisha kuwa yapo madhara makubwa yanayotokana na kelele ikiwemo maradhi ya saratani, shinikizo la damu na kisukari ambayo endapo hatua zisipochukukuliwa wananchi wataendelea kuathrika.

Pia, alisema pamoja na kuwasaidia wajasiriamali kujipatia kipato, baadhi ya matangazo holela ya biashara ndogondogo mitaani kwa kutumia vipaza sauti bila mpangilio yamekuwa chanzo cha uchafuzi wa mazingira kwa kelele hivyo yanapaswa kuwekewa utaratibu mzuri.

“NEMC tuchuke hatua kwakuwa sheria, kanuni na miongozo inayoelezea namna ya kuzuia uchafuzi wa mazingira hasa kelele ipo, leo hii ukipita mtaani nyumba 100 au 200 asilimia 20 zina kelele na mitetemo na muziki, nawaagiza mkae na TAMISEMI mje na mkakati wa kutatua changamoto hii,“ alisisitiza.

Kwa upande mwingine aliwapongeza watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Taasisi yake ya NEMC kwani wanategemewa na wananchi katika kusimamia Mazingira ambayo ni sekta pana na yenye mambo mengi yanayomzunguka mwanadamu.

Halikadhalika, alisema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imepewa dhamana kubwa ya kutekeleza Nguzo ya Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu wa Mabadiliko iliyopo katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Hivyo, katika kufikia Dira hiyo aliwataka watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuleta matokeo kwani karibu Wizara zote zinategemea usimamizi wa mazingira chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais yaliyohufadhiwa

Awali akimkaribisha Mhe. Naibu Waziri, Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Mhandisi Mwanasha Tumbo alimpongeza kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu hassawakushika wadhifa huo.

Alisema kuwa mazingira ni suala mtambuka hivyo kuteuliwa kwa Mhe. Dkt. Dugange ambaye awali alikuwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI atakuwa chachu katika kuchagizi uhifadhi wa mazingira.

Vilevile Mhandisi Mwanasha alisema kuwa Baraza linakusudia kuwa na mpango wa miaka mitano wa kuchukua yaliyomo kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ambayo yataakisi shughuli zake.

Alifafanua kuwa kupitia shughuli hizo ndani ya mpango huo utaonesha umuhimu wa kuipa NEMC Mamlaka kamili na kuwa Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) kama ambavyo mchakato unavyoendelea.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Semesi alitoa ufafanuzi kuhusu majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na Baraza hilo kupitia Idara na Vitengo mbalimbali.

Alisema kuwa utoaji vyeti hufanyika kupitia michakato mbalimbali ambapo maafisa hufika maeneo ambayo miradi hutarajiwa kutekelezwa na kukutana na wadau ambao wanatarajia kutekeleza miradi.

Dkt. Semesi alisema kuwa baada ya kupitia michakato hiyo vyeti hupelekewa kupelekwa wizarani (Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira) kwa ajili na kuhakikiwa ili Mheshimiwa Waziri wa Nchi aridhie kuvisaini kisha kutolewa.

Hii ni ziara ya kwanza ya Naibu Waziri Dkt. Dugange ya kutembelea moja ya taasisi zilizopo chini ya ofisi ya Makamu wa Rais, tangu ateuliwa kushika wadhifa huo

Settings