‘Kilimo kisijumuishwe katika sekta zinazotakiwa kupunguza gesi joto’

Oct, 11 2021

Tanzania inapendekeza sekta ya kilimo isijumuishwe katika sekta zinazotakiwa kupunguza gesi joto kwa kuwa kilimo kinaathirika na athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na kutegemea mvua.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 11, jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo wakati akitoa Tamko la Serikali kuhusu msimamo wa Tanzania kwenye majadiliano ya Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.

Jafo alisema mchango wa uzalishaji wa gesi joto utokanao na shughuli za kilimo ni mdogo katika nchi zinazoendelea ukilinganisha na nchi zilizoendelea na hivyo kumekuwa na maoni kinzani kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea kuhusu kujumuisha sekta ya kilimo katika sekta zinazotakiwa kupunguza uzalishaji wa gesijoto.

Alisema nchi zinazoendelea kama Tanzania ili ziweze kujiimarisha kwa ufanisi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi, zinahitaji kujengewa uwezo katika kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa kwenye Mkataba na Makubaliano ya Paris.

“Msimamo wa Tanzania katika suala hili ni kuzitaka nchi zilizoendelea pamoja na mashirika ya kimataifa kutilia mkazo suala la kujenga uwezo wa nchi zinazoendelea ili ziweze kutoa mchango wake katika kupunguza uzalishaji wa gesijoto duniani,” alisema Waziri Jafo.

Aidha, kwa mujibu wa Mkataba huu, nchi zilizoendelea ziliahidi kutoa kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 100 kila mwaka ifikapo mwaka 2025 ili fedha hizi ziwezeshe nchi zinazoendelea kama Tanzania kuweka mipango na mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.

Hivyo alisema msimamo wa Tanzania katika suala hili ni kuzitaka nchi zilizoendelea kutimiza wajibu wao wa ahadi ya kutoa fedha hizi kama ilivyokubaliwa.

Kuhusu mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Jafo alifafanua kuwa Makubaliano ya Paris yanaitaka kila nchi mwanachama kuandaa Mchango wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo Tanzania iliwasilisha mchango wake kwenye sekretarieti ya Mkataba tarehe 30 Julai 2021.

“Msimamo wa Tanzania katika suala hili ni kwamba Mkutano huu ufikie maamuzi yatakayowezesha upatikanaji wa fedha za kuwezesha nchi zinazoendelea kutekeleza michango yao na kwamba mapitio ya michango hiyo yafanyike kila baada ya miaka mitano,” alisema.

Aliongeza kuwa suala la upunguzaji wa gesijoto kwenye uso wa dunia halina budi kufanyika ili ongezeko la joto liwe chini ya nyuzi joto 20C na pia juhudi za ziada zinahitajika ili ongezeko lisivuke nyuzi joto 1.50C kwa ajili ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema Makubaliano ya Paris kwenye kipengele cha 6 yanatoa fursa ya nchi mbalimbali kushirikiana kwenye upunguzaji wa gesijoto kwa kutumia mbinu ya biashara.Hivyo Msimamo wa Tanzania ni kwamba nchi inayouza ziada ya upunguzaji isijumuishe kiwango kilichouzwa kwenye orodha yake ya upunguzaji ili kusitokee kuhesabiwa mara mbili kwani nchi iliyonunua ziada hiyo ndiyo itaweka kiwango hicho kwenye orodha yake ya upunguzaji gesijoto.

Settings