Naibu Waziri Khamisi awataka viongozi wa mikoa kutoa elimu ya upandaji miti

Oct, 11 2022

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.Khamis Hamza Khamis amewataka viongozi wa mikoa na wilaya nchini kutoa elimu ya upandaji miti kwa wananchi.

Amesema rai hiyo wakati wa ziara ya Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta kupeleka mrejesho wa Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 iliyofanyika mkoani Rukwa Oktoba 11, 2022.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo amewataka viongozi hao kwenda kuelimisha wananchi namna bora ya kutunza vyanzo vya maji na kueleza kuwa changamoto kubwa iliyopo kwenye vyanzo hivyo ni shughuli kubwa za kibinadamu.

Alisema maeneo mengi yanayovamiwa wavamizi wake hawaendi tu kuvamia bali wanakata na miti na kuharibu vyanzo vya maji ambapo aliwataka viongozi wa mikoa na wilaya kuwaeleza wananchi ambao vijiji vyao vitabaki basi wapande miti.

Aidha, naibu waziri huyo aliwataka wananchi nchi nzima kushiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji wa miti na kuitunza ili iweze kukua na hivyo mazingira kuhifadhiwa.

Kuhusu suala la utumzaji vyanzo vya maji, alisema mbali na uchafuzi wa mazingira unaofanywa kwenye maeneo yaliyovamiwa lakini wengine wanaharibu kwa kujenga nyumba na mwisho wa siku wanaharibu mazingira.

“Kikubwa sisi kazi tuliyokuwa nayo ni kwenda kuwaambia wananchi waende wakaheshimu na kutunza vyanzo vya maji na shughuli zetu za kibinadamu zisiharibu mazingira," Mhe. Khamis.

Ziara hiyo ya mawaziri hao itaendelea Mkoa wa Katavi 12 Oktoba 2022 kabla ya kuelekea Kigoma Oktoba 13, 2022.

Settings