Katibu Mkuu Maganga: Serikali yakaribisha wawekezaji hewa ya ukaa

Apr, 08 2022

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi Mary Maganga amesema Serikali inakaribisha wawekezaji katika utekelezaji wa miradi ya kupanda miti na biashara ya hewa ukaa nchini ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi na changamoto za upotevu wa misitu.

Amesema hayo alipokutana na ujumbe wa Kampuni ya Carbon Planet Ltd iliyowaailisha taarifa kuhusu maeneo inayoweza kushirikiana na Tanzania katika shughuli za biashara ya hewa ukaa na upandaji miti ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi na changamoto za upotevu wa misitu.

Bi. Maganga aliishukuru kampuni hiyo na kuiasa iwasilishe rasmi andiko la mradi husika Serikalini ili liweze kufanyiwa kazi, hususan maombi ya kupatiwa idhini ya kushiriki katika biashara ya hewa ya ukaa.

katika mawasilisho yake kampuni hiyo ilibainisha kuwa inajihusisha na shughuli za kupanda miti ya mitiki kwa ajili ya biashara ya hewa ukaa na mbao.

Ilibainisha kuwa hadi sasa kampuni hiyo imepanda hekari 30,000 za mashamba ya miti ya mitiki wilayani Kibiti mkoani Pwani sambamba na biashara ya hewa ukaa kwa lengo la kuchangia katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hivyo, kampuni hiyo iko tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza Mchango wa Taifa wa Kukabliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC) na Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2021.

Ilisema katika utekelezaji wa mipango na mikakati hii, Kampuni ya Carbon Planet itakuwa tayari kujenga uwezo wa wananchi, taasisi na watalaamu wanaohusika na upandaji wa misitu na biashara ya hewa ukaa ili kuchangia katika jitahada za kimataifa za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Katika kikao hicho Ujumbe wa kampuni hiyo uliongozwa na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wake Bw. Amin Lakhani na Mtalaamu wa masuala ya Biashara ya Hewa Ukaa na Misitu kutoka India Dkt. Chakal na Rajesh.

Settings