Katibu Katibu Mkuu Mitawi ahimiza Watanzania kulinda Muungano

Aug, 03 2025

Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuulinda na kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwani umeleta faida lukuki.

Ametoa wito huo wakati alipotembelea banda la Ofisi ya Makamu wa Rais kwenye Maonesho ya 32 ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma, leo Agosti 03, 2025.

Bw. Mitawi amewahimiza wananchi kutumia fursa ya uwepo wa maonesho hayo kufika katika viwanja hivyo na kutembelea banda hilo ili kujifunza masuala mbalimbali kuhusu Muungano huo adhimu.

Aidha, alisema ni muhimu Watanzania wakatambua kuwa tangu Aprili 26, 1964 hadi sasa Muungano umekuwa na Mambo 22 yaliyopo Tanzania Bara na Zanzibar hivyo, wakitembelea banda hilo watajifunza na kupata uelewa zaidi.

Halikadhalika, Bw. Mitawi alisema kuwa Muungano una historia kubwa na waasisi wake Hayati Mwalimu Juluus Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Aman Karume walikuwa na sababu ya kuziunganisha nchi hizo mbili ikiwemo udugu miongoni mwa wananchi wao.

“Nawakaribisha wananchi wote watembelee banda letu na watakapokuja watapata kufahamu mambo mbalimbali ambayo Ofisi inayafanyia kazi na tunatambua kuwa tunasimamia mambo makuu matatu ambayo ni Muungano, Mazingira na Uchumi wa Buluu,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu Mitawi aliongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo inasimamia masuala makuu matatu yakiwemo Muungano, Mazingira na Uchumi, pamoja na kutoa elimu kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii pia inaendelea kuwaelimisha wananchi wakati wote huu wa Maonesho ya Nanenane.

Hivyo, yapo mengi ya kujivunia kutokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo yameleta manufaa makubwa yakiwemo upatikanaji wa huduma za kijamii, kukua kwa fursa za kibiashara na kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo katika pande zote mbili za Muungano.

Maonesho ya Nanenane kwa mwaka 2025 yanachagizwa na kaulimbiu isemayo Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo endelevu ya Kilimo, Mifugo na uvuvi 2025 ambapo yalifunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango Agosti mosi, 2025 na kutarajiwa kuhitimishwa Agosti 08, 2025.

Settings