Jafo: Nchi zilizoendelea zitimize wajibu wao kukabali mabadiliko ya tabia nchi

Nov, 05 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Selemani Jafo amesema Athari za mabadiliko ya Tabianchi zinaonekana dhahiri katika maeneo mbalimbali nchini na kusema kuwa ipo haja ya kuongeza jitihada za dhati katika kukabiliana nayo.

Waziri Jafo ameyasema hayo hii leo mjini Glasgow Scotland katika Mkutano wa 26 wa Nchi waWanachama wa Mkataba wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.

Amezitaja athari hizo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari kulikosababisha kisiwa cha Maziwe Wilaya ya Pangani na kisiwa cha Fungu la Nyani Wilaya ya Rufiji kumezwa na maji ya bahari na kuongezeka kwa kina cha maji kwenye Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.

“Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi Ili kukabiliana na athari hizi ambazo zinatishia kurudisha nyuma juhudi za serikali za miongo kadhaa za kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa watu wake” Jafo alisisitiza.

Amesisitiza kuwa katika mkutano unaoendea viongozi wa mataifa makubwa ambayo kwa kiasi kikubwa mataifa yao ndio chanzo cha uzalishaji wa hewa ya ukaa wameonyesha nia ya dhati ya kutekeleza makubaliano waliojiwekea ya kutoa fedha kwa wakati ili kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

Amesema mataifa hayo yanawajibika kutokana na makubaliano ya Mkataba wa Paris ambao unazitaka nchi zilizoendelea kutoa kiasi cha Dola Bilioni Mia moja kila mwaka kwa nchi zinazoendelea ili ziweze kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi.

“Tunadhamiria na kusisitiza kuwa sasa tutoke kwenye maneno na twende kwenye vitendo, wenye jukumu la kutoa fedha watoe ili miradi mbalimbali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi iweze kutekelezeka kwa wakati” Jafo alisisitiza.

Waziri Jafo amesema katika kuungana na Jumuiya ya Kimataifa kupunguza uzalishaji wa gesijoto, Tanzania pia imechukua hatua stahiki zikiwemo Kuandaa Mpango wa Taifa wa Kupunguza Gesijoto (2021 - 2026); Kuimarisha usimamizi wa misitu na program za upandaji miti; kuendelea na ujenzi wa Mradi wa umeme wa Bwawa la Mwl Nyerere; Ujenzi wa Reli ya kisasa; kuanza kutumika kwa gesi majumbani na kwenye uendeshaji wa mitambo viwandani na kwenye magari badala ya dizeli na petroli na Mfumo wa usafiri wa mabasi yaendayo kasi katika jiji la Dar es salaam ambavyo vinachangia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza Rais (Zanzibar) Dkt. Saada Mkuya amesema athari za mabadiliko ya tabianchi ni kubwa kwa upande wa Zanzibar kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari na kusabisha baadhi ya visiwa kutoweka na baadhi ya maeneo ya ardhi kuingiwa na maji chumvi na kuathiri shughuli za uzalishaji hususan kilimo na uvuvi hivyo kuathiri uchumi.

Awali Waziri Jafo na Waziri Dkt. Saada Mkuya wamekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Prof.Petteri Taalas na kuzungumzia masuala ya kuhimili mabadiliko ya Tabianchi ambayo ni changamoto kubwa kwa sasa duniani.

Mkutano wa 26 wa Nchi wa wanachama wa Mkataba wa Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaendelea Glasgow, Scotland na utamalizika tarehe 12 Novemba 2021.

Settings