​Jafo: Hoja za Muungano zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu

Aug, 23 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo amesema hoja mbalimbali za Muungano zinaendelea kushughulikiwa na Kamati ya Pamoja ili kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Akizungumza mara baada ya ziara ya wajumbe wa Kamati hiyo walipotembelea kiwanda cha Maziwa Fumba na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume katika jengo la (Terminal III).

Amesema miradi hiyo ya kimkakati ni miongoni mwa hoja za Muungano ambazo zinatafutiwa ufumbuzi na kamati ya pamoja ili kuhakikisha ufumbuzi unapatikana kwa lengo la kuimarisha umoja uliopo.

Aliwataka wananchi wafahamu kuwa serikali zote mbili bado zinaendelea kukaa pamoja na kujadili hoja mbalimbali za muungano kwa maslahi ya wananchi.

Nae waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba amesema tayari hoja mbalimbali katika masuala ya fedha zimepatiwa fumbuzi ikiwemo suala la fedha kutoka uhamiaji na kodi ya ongezeko la thamani.

Alieleza kuwa ulipaji wa kodi upande mmoja unamuwezesha mwananchi kupata unafuu na kurahisisha mzunguko wa biashara nchini.

Alisema juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha Viwaja vya Ndege ni muhimu kwa maendeleo kwani majengo ya kisasa yanasaidia katika kuimarisha sekta ya utalii nchini.

Aliwataka wanachi kuendelea kushirikiana na viongozi wao katika kutunza miundombinu ili waweze kuimarisha zaidi viwanja vya ndege kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.

Settings