Jafo atoa siku 14 mradi wa machinjio Kigoma kusajiliwa

May, 13 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo ametoa siku kumi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma kuhakikisha anasajili mradi wa ujenzi wa Machinjio ya kisasa ili uweze kupata cheti cha Tathmini ya Mazingira.

Akiwa katika siku ya pili ya ziara yake Mkoani Kigoma Waziri Jafo ametembelea machinjio ya Manispaa ya Kigoma na kubaini ujenzi unaendelea bila kufuata taratibu za kimazingira kwa kuwa hauna Cheti cha Tathmini ya Athari ya Mazingira.

"Naagiza mradi huu usajiliwe mapema iwezekanavyo, na lengo la kufanya hivi si kupata cheti tu bali muhimu ni kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala muhimu ya kuzingatia katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira" Jafo alisisitiza

Waziri Jafo amesema endapo Manispaa ya Kigoma itashindwa kusajili mradi huo wa machinjio ya kisasa kwa kipindi tajwa atasitisha ujenzi huo.

"Hivi sasa kuna mfumo wa kusajili miradi kwa njia ya mtandao na miradi yote naiona hapa kwenye tablet yangu sasa ikifika tarehe 25/05/2021 sijaona mradi wenu nitasitisha ujenzi wenu" Jafo alisisitiza.

Pia, Waziri Jafo amewataka wawekezaji kote nchini kusajili miradi yao ili iweze kukidhi vigezo vya kupatiwa cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira kinacho ainisha namna bora ya kupunguza madhara ya kimazingira yatikanayo na utekelezaji wa miradi.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo amesema azma ya Serikali ni kuhakikisha inahamasisha wawekezaji kuwekeza katika uzalishaji wa nishati mbadala ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Waziri Jafo ameyasema hayo mara baada ya kutembelea Mradi wa Nishati ya Jua na kuridhishwa na uzalishaji rafiki kwa mazingira ambao uzalisha kiasi Mega Watt 1 kwa sasa huku lengo likiwa ni kuzalisha Mega Watt 4.8 kufikia 2025.

Amesema umeme unaozalishwa kutoka katika Mini-grid ya Kigoma unafaida kubwa kimazingira kwa kuwa unapunguza matumizi ya umeme wa Mafuta ambao gharama yake ni kubwa na kupongeza Uongozi wa Mkoa wa Kigoma kwa kutumia Green Power.

Settings