Habari
Dkt Muyungi ahimiza mazoezi kwa watumishi
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amewahimiza watumishi wa Ofisi hiyo kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya ya mwili na akili.
Dkt. Muyungi ametoa rai hiyo aliposhiriki mazoezi ya viungo na mbio fupi yaliyojumuisha baadhi ya wajumbe wa menejimenti na watumishi hao yaliyofanyika leo Mei 09, 2026 jijini Dodoma.
Alisema kuwa amefarijika kuona idadi kubwa ya watumishi wakishirikikatika mazoezi hayo yanayofanyika kila Jumamosi ambayo pamoja na kusaidia kukijikinga na maradhi lakini pia yanaimarisha ufanisi katika kazi.
“Nimeona mlivyofika kwa wingi katika mazoezi haya na hii inadumisha urafiki na Muungano kwani hapa tumekutana watumishi wa kila Idara na Vitengo nami naahidi nikipata nafasi ntakuwa nafika hapa kujumuika nanyi katika mazoezi,” alisisitiza Dkt. Muyungi.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Dkt. Muyungi alieleza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuboresha mazingira ya michezo kwa watumishi ili waweze kushiriki kikamilifu katika michezo.
Kwa kuzingatia hiyo, Ofisi tayari imeshanunua eneo kwa ajili ya kujenga uwanja wa michezo lililopo Ipala jijini Dodoma ambao pindi ukikamilika utakuwa chachu kwa watumishi hao katika kuimarisha ushirikiano na taasisi zingine kupitia sekta.
Kwa upande wake Katibu wa Michezo Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Marwa Nyaisawa kwa niaba ya watumishi alisema anamshukuru Katibu Mkuu kwa kujumuika katika mazoezi hayo.
Alisema kuwa ushiriki wa kiongozi huyo katika mazoezi utaongeza ari ya kushiriki katika michezo yakiwemo mashindano mbalimbali ambayo timu za Ofisi zinaposhiriki.
Hivyo, Bw. Marwa aliwasihi watumishi wenzake waendelee kushiriki kikamilifu katika michezo ili kujiimarisha na hivyo kukuza ufanisi ambao utaleta matokeo chanya kwenye sekta hiyo.



