Dkt. Mpango: Serikali kuendelea kuhuisha viwango vya mishahara

May, 01 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali itaendelea kuhuisha viwango vya mshahara kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi na kibajeti pamoja na ujuzi na utendaji wa waajiriwa ili kuepuka kuchochea mfumuko wa bei, kuhatarisha uhimilivu wa deni la Taifa na athari nyingine kwenye utulivu wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mkoani Arusha tarehe 01 Mei 2024. Amesema changamoto mbalimbali ambazo zimeikumba dunia ikiwemo vita na majanga ya asili zimeendela kuathiri uchumi wa Taifa kutokana na kuvurugika kwa mfumo wa ugavi na kupanda kwa bei za mafuta, mbolea, chuma na chakula.

Makamu wa Rais amesema Pamoja na changamoto hizo tathmini ya Serikali na ya Taasisi za kimataifa ikiwemo IMF, Benki ya Dunia, AfDB, Moody’s, Fitch na zinginezo zimeonesha kuwa uchumi wa Taifa umekuwa stahimilivu kwa kiasi cha kuridhisha hivyo hali hiyo itakapoendelea kudumu wafanyakazi wawe tayari kunufaika.

Aidha amesema Serikali imeendelea kuboresha maslahi ya watumishi kwa namna mbalimbali, ikiwemo kwa kulipa nyongeza ya mwaka ya mshahara ambapo Mwaka 2023/24 kiasi cha shilingi bilioni 153.9 kililipwa na kwa mwaka 2024/25, Serikali imetenga shilingi bilioni 150.8 kwa ajili hiyo. Pia amesema Serikali imeendelea kuwapandisha vyeo watumishi mbalimbali, ambapo Mwaka 2023/24 jumla ya watumishi 81,515 walipandishwa vyeo na mwaka 2024/25 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 252.7 kwa ajili ya kuwapandisha vyeo watumishi 219,924.

Makamu wa Rais amesema serikali inathamini na kupokea hoja ya kuboresha Kanuni ya ukokotoaji wa mafao ambapo suala hilo ambalo ni la sayansi ya Watakwimu-bima litashauriwa kwa kuzingatia uhimilivu na uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema likizo ya uzazi ni haki ya mfanyakazi na iwapo mfanyakazi atajifungua mtoto au watoto njiti, kipindi cha uangalizi maalumu hakitahesabiwa kama likizo ya uzazi. Amesema vilevile mfanyakazi husika ataruhusiwa kutoka kazini saa 7:30 kila siku kwa muda wa miezi sita baada ya kumalizika kwa likizo ya uzazi ili kumpa fursa ya kwenda kunyonyesha. Aidha amesema Serikali ipo katika hatua ya kuifanyia marekebisho Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, Sura 366 ili likizo ya uzazi ianze pale mtoto atakapomaliza kipindi cha uangalizi maalum kadri madaktari watakavyothibitisha.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa wafanyakazi nchini kuendelea kutekeleza majukumu kwa bidii, maarifa, uadilifu kwa kutanguliza maslahi ya Taifa mbele kwa kuongeza tija katika utendaji kazi. Amevisihi vyama vya wafanyakazi kushirikiana na Serikali na Waajiri kuhakikisha tija inaongezwa kwenye maeneo ya kazi kwa manufaa ya Taifa na wafanyakazi wenyewe.

Aidha amewaasa wafanyakazi kuwa mstari wa mbele katika kudai risiti kila wanaponunua bidhaa na kuhakikisha risiti wanazopewa zimeandikwa gharama halisi ili kuiwezesha Serikali kupata mapato zaidi na kupelekea wigo mpana zaidi wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Maadhimisho ya Mei Mosi kitaifa yamehuduhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko, Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Deogratius Ndejembi, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Dkt. Moses Kusiluka, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) Tumaini Nyamhokya, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi John Mongela, Viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini, Mahakama, Vyama vya Wafanyakazi pamoja na wafanyakazi sekta binafsi na serikali.

Settings