Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya tathmini ya Mashirika yanayojiendesha kwa hasara na itachukua hatua stahiki kulingana na taarifa ya tathmini inayofanyika.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 12 Agosti 2022 wakati wa hafla ya miaka 50 ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) iliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Ametoa wito kwa Mashirika mengine ya umma kuiga mfano wa STAMICO ambapo huko nyuma Shirika lilikuwa linasuasua kiutendaji lakini sasa limeanza kujikwamua.
Aidha Makamu wa Rais amaitaka Wizara ya Madini, STAMICO na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuongeza kasi ya ukaguzi wa migodi mikubwa na midogo ili kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wachimbaji madini wanaozembea na kuharibu au kuchafua mazingira. Amasema elimu ya kutosha inapaswa kutolewa juu ya madhara makubwa ya uchafuzi wa mazingira kwa maisha ya binadamu na viumbe vingine hai na uendelevu wa ikolojia. Ameitaka Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na Wizara ya Afya kuhakikisha sheria na kanuni za afya na usalama mahala pa kazi zinafuatwa ili kuondokana na changamoto ya ongezeko la idadi ya wagonjwa kutoka katika migodi ya madini ambao wanaathirika na vumbi linalotokana na shughuli za uchimbaji.
Pia Makamu wa Rais ametoa rai kwa taasisi za fedha kuendeleza jitihada za kuweka masharti nafuu ya upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo na wa kati ili kuwasaidia kupata mitaji na zana za kisasa zitakazo wawezesha kuongeza tija, ajira na kufanya shughuli za uchimbaji kwa kutumia teknolojia rafiki na mazingira yanayowazunguka.
Makamu wa Rais amesema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea na jitihada za kuboresha sekta ya Madini na kuhakikisha inakua kwa kasi kubwa, inatoa ajira kwa watanzania wengi zaidi na kuchangia zaidi katika pato la Taifa.
Waziri wa Madini Dkt. Dotto Biteko amesema shirika la madini la taifa linapaswa kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza ushindani duniani na sio Tanzania pekee. Amelipongeza shirika hilo kwa ubunifu wakati wa kukabiliana na changamoto za taratibu za manunuzi zilizokuwa zinajitokeza.
Kwa Upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amesema kwa sasa utekelezaji wa kuzingatia kila jambo linalofanyika kuendana na sera za mazingira unafanyika kwa kasi kubwa na kuwapongeza STAMICO kwa kuanzisha mkaa mbadala ambao utasaidia katika kupunguza gesi joto duniani. Amewaasa kuhakikisha uzalishaji wa mkaa huo unaongezeka ili watanzania waweze kutumia na kusaidia katika utunzaji mazingira.
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya STAMICO Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Shirika hilo Dkt. Venance Mwasse amesema shirika limepata mafanikio ikiwemo kuongezeka kwa mapato na kuacha utegemezi serikalini kwa asilimia 100, kuimarisha miradi ya uchorongaji kwa kununua mitambo mipya, kufufua mradi wa makaa ya mawe kiwira, kuendeleza wachimbaji wadogo pamoja na kuanzisha kiwanda cha kuongeza thamani ya madini jijini Mwanza. Amesema STAMICO inatarajia kununua mitambo kumi kwaajili ya wachimbaji wadogo pamoja kuendelea kuwasaidia wachimbaji wenye mahitaji maalumu.
Katika hafla hiyo, Makamu wa Rais amezindua Mitambo ya kisasa ya uchorongaji na uchimbaji madini ya STAMICO yenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 pamoja na kuzindua mkaa mbadala kutoka katika shirika hilo wenye jina la Rafiki Briquettes. Pia Shirika hilo limetoa shilingi bilioni 2.2 kwa serikali ikiwa ni gawio kutoka na mapato yaliopatikana katika mwaka wa fedha 2021/2022