Dkt. Mpango: Benki ziwakoshe vijana

May, 19 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Mabenki hapa nchini kuendelea kubuni madirisha maalum ya mikopo kwa vijana na wanawake ambao huchukuliwa kuwa ni soko gumu kwa huduma za fedha licha ya kwamba ndio sehemu kubwa ya nguvukazi ya taifa.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Ufunguzi wa Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB inayofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) leo tarehe 19 Mei 2023. Amewahimiza kuweka mkakati wa namna ya kulifikia soko la vijana na wanawake ili kusaidia nchi kupiga hatua kubwa zaidi kiuchumi.

Aidha Makamu wa Rais ametoa wito wa kushughulikiwa kwa changamoto ya masharti magumu na riba kubwa za mikopo ambazo ni kikwazo kwa walio wengi kuweza kunufaika na mikopo. Pia amesema ni asilimia 8.6 tu ya wananchi waishio vijijini wanapata huduma za benki kwa sasa hivyo ipo sababu ya kuongeza kasi ya kuwafikia wananchi waishio maeneo hayo pamoja na kupunguza riba kuwafikia wachimbaji wadogo, wafugaji na wavuvi.

Halikadhalika amezisihi benki za biashara kuendelea kuhakikisha zinazingatia ufanisi katika utendaji ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji, kuongeza matumizi ya TEHAMA na kuongeza juhudi katika kupunguza mikopo chechefu.

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya maboresho ya mazingira ya biashara nchini kupitia utekelezaji wa Mpango wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara (Blueprint) ambapo baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na serikali kupunguza urasimu na majukumu kinzani katika taasisi za umma na kupunguza baadhi ya kodi na tozo zisizo na tija. Pia amesema Serikali imeendelea kutekeleza Sera za Bajeti na Fedha zinazolenga kuwezesha sekta binafsi ambapo hatua hizo ni pamoja na kulinda thamani ya shilingi na kuhakikisha akiba ya fedha za kigeni ni toshelevu na kupunguza kiwango cha serikali kukopa kutoka benki za biashara za ndani ili kuzipa fursa benki hizo kufadhili zaidi sekta za uzalishaji.

Makamu wa Rais amesema serikali itaendelea kuboresha na kuweka mazingira rafiki kwa sekta ya fedha na sekta binafsi kwa ujumla ili kuongeza uwekezaji na kuchochea ukuaji wa pato la taifa. Ameipongeza Benki ya CRDB kwa mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo pamoja na mambo mengine bei ya hisa imeongezeka kutoka Shilingi 145 mwaka 2018 hadi kufikia Shilingi 440 mwishoni mwa mwaka 2022.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema Benki hiyo imejipanga kupitia kuwekeza katika ubunifu wa huduma , bidhaa zitakazosaidia kuboresha Maisha ya watanzania waliowengi pamoja na kukuza uchumi wa taifa. Amesema Benki imelenga kuhakikisha kasi ya mabadiliko kila wakati inaendana na mabadiliko ya mahitaji ya wateja na watanzania kwa ujumla.

Nsekela amesema Benki hiyo inazingatia masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika utendaji kazi na utaoaji huduma ili kuhakikisha nchi inakua salama

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay ametoa wito kwa watanzania kujenga tabia ya kuwekeza kwenye hisa kwani katika taifa muamko ni mdogo sana katika masuala ya uwekezaji katika hisa kuliko rasilimali zingine. Amesema ni wakati muafaka wa kuongeza katika mitaala ya elimu masuala ya his ana soko lake ili vijana waweze kupata ufahamu wa mambo hayo wakiwa bado wadogo.

Settings