Dkt.Mpango awataka wazalishaji viwandani kuongeza thamani ya bidhaa ghafi

Nov, 18 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wazalishaji wa viwandani hapa nchini kufanya jitihada na kuongeza thamani ya bidhaa ghafi zinazopatikana hapa nchini ili kuondokana na nchi kupata mapato kidogo ya fedha za kigeni na kupoteza ajira za idadi kubwa ya watu nchini.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Hafla ya Utoaji Tuzo za Rais za Wazalishaji Bora viwandani zilizofanyika katika ukumbi wa Serena Jijini Dar es salaam leo tarehe 18 Novemba 2022.

Amesema takribani asilimia 12 ya fedha za mauzo nje ya nchi (export earnings) zinatumika kulipia uagizaji wa bidhaa za walaji (consumer goods) ambazo nyingi zinaweza kuzalishwa hapa nchini na kukidhi mahitaji ya ndani na hivyo kupunguza upotevu wa rasilimali ya fedha za kigeni.

Aidha Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji hapa nchini ikiwemo kufanya maboresho zaidi ya kitaasisi, sheria, sera za fedha na bajeti ambapo hadi sasa zaidi ya kodi na tozo 230 zisizo na tija zimefutwa na takribani sheria na miongozo 40 imeboreshwa na majukumu ya baadhi ya taasisi yameendelea kuboreshwa ili kuongeza ufanisi.

Katika kuhakikisha biashara inaendelea kukua nchini, Makamu wa Rais amesema serikali imeendelea kuboresha na kuongeza ufanisi wa Bandari, kuboresha sekta ya Nishati pamoja na Miundombinu ikiwemo nia yakuiunganisha reli ya kisasa ya SGR na nchi jirani kama Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kuchochea biashara ya kikanda na kuwezesha Taifa kunufaika na huduma na usafirishaji wa madini na bidhaa mbalimbali kutoka katika nchi hizo.

Pia Makamu wa Rais amesema Serikali kwa kushirikisha wadau inaendelea kushughulikia changamoto ya tozo kubwa ya stempu za kielotroniki kwa lengo la kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa gharama ndogo zaidi. Aidha amesema serikali imeboresha mkakati wa kusimamia madeni ya wazabuni na inaendelea kulipa malimbikizo ya madai ya waliotoa huduma Serikalini ambapo kwa kipindi cha Julai – Oktoba 2022 pekee, zaidi ya shilingi bilioni 420 zimeshalipwa huku ikipunguza kwa asilimia 74madeni ya ushuru wa forodha wa ziada kwa waingizaji wa sukari ya viwandani na asilimia 32 ya deni la Ongezeko la Thamani (VAT refunds).

Settings