Dkt. Mpango awaasa Watanzania kuwaunga mkono wajasiriamali wa ndani

Jul, 13 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 13 Julai 2022 amefunga Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Sabasaba yaliofanyika Jijini Dar es salaam kuanzia tarehe 28 Juni 2022.

Katika hotuba yake wakati wa ufungaji wa Maonesho hayo, Makamu wa Rais amewaasa wazalishaji hapa nchini kuzingatia kanuni za ushindani katika soko, ikiwemo kuheshimu mikataba na kuzalisha bidhaa bora na za viwango vya juu pamoja na uzalishaji wa bidhaa ambazo zina mahitaji makubwa nchini kama vile chakula na bidhaa za ujenzi. Aidha amewahimiza watanzania kuendelea kuunga mkono bidhaa za wajasiriamali wa ndani kwa kununua bidhaa hizo.

Makamu wa Rais amesema watanzania hawana budi kujipanga ili kutumia kikamilifu eneo huru la kibiashara la Afrika (AfCTA) lenye takriban watu bilioni 1.3. katika kuudha bidhaa na kuongeza wigo wa soko la bidhaa za Tanzania. PaiaamewatakaTanTrade na Wizara zinazohusika na Biashara Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa elimu zaidi ya masoko kwa wafanyabiashara ili waweze kuchangamkiana kunufaika na fursa hizo.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amewaasa wafanyabiashara, wenye viwanda na wananchi wote kuhakikisha wanalinda Mazingira kwa kutunza ekolojia , misitu, kupanda miti na kufanya usafi wa mazingira katika maeneo ya biashara na maeneo ya uzalishaji viwandani wakati wote. Aidha amewasihi wananchi wote kushikriki Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23 mwaka 2022 kitakayorahisisha mipango ya maendeleo ya Taifa.

Awali akitembelea Mabanda mbalimbali katika maonesho hayo Makamu wa Rais amewasihi watoaji huduma za kifedha yakiwemo mabenki kuendelea kupunguza riba ili kuwapa fursa wajasiriamali wadogo kupata mitaji na kufanya biashara. Aidha ameigiza Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara kuwatafutia maeneo maalum ya kufanyia biashara watu wa makundi maalum wakiwemo wasioona.

Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema wizara itahakikisha Tanzania inaenda katika eneo huru la kibiashara la Afrika kama washindani na sio washiriki. Aidha Dkt. Kijaji amesema katika maonesho ya 46 ya kimataifa ya sabasaba wizara imeanzisha kliniki ya bishara ambapo taasisi 20 za serikali zilitoa ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za wafanyabiashara Pamoja na wawekezaji. Amesema Kliniki imehudumia wadau 93 na changamoto 120 zimepatiwa suluhisho papo kwa papo.

Kwa upande wake Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Omar Said Shaaban amesema serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaunga mkono jitihada za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika harakati za kuboresha mazingira bora ya biashara na kuwekeza katika viwanda inayochochea uzalishaji na kupatikana ajira na kukuza uchumi kwa ujumla kwa kuzingatia maeneo mapya ya kiuchumi katika viwanda.

Awali akitoa taarifa ya mwenendo wa maonesho hayo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania Latifa Khamis amesema katika maeonesho hayo kumekuwepo na ongezeko la ushiriki kutoka kampuni 3200 kwa mwaka 2021 mpaka 3425 kwa mwaka 2022. Amesema Tantrade itaendelea kutoa mchango wake ili kuhakikisha sekta ya biashara nchini inasaidia ukuaji wa uchumi wa Taifa. Amesema wataendelea kuboresha maeesho hayo ili kuwa na tija stahiki katika kupata masoko ya bidhaa mbalimbali hususani zinazozalisha nchini.

Settings