Dkt. Mpango ashuhudia kusainiwa kwa hati za makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi

Aug, 24 2021

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango hii leo ameshuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi. Hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii,Maruhubi, Zanzibar.

Hafla hiyo imehudhuriwa na na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Abdullah, Katibu Mkuu Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Hussein Katanga, Katibu wa Mkuu Kiongozi Zanzibar Mhandisi Zena Said, Mawaziri, Makatibu wakuu kutoka pande zote za muungano pamoja na viongozi wengine.

Akizungumza katika Hafla hiyo, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema utaratibu wa kutafuta ufumbuzi wa hoja za muungano kupitia mazungumzo una nia ya kuuenzi na kuulinda muungano thabiti uliopo. Aidha ametoa rai kwa taasisi zote husika kuwa kuhakikisha changamoto zinazoendelea kutafutiwa ufumbuzi na zile zitakazojitokeza, ni muhimu kuzitambua mapema, kuzijadili kwa uwazi na umakini ili kuzitafutia ufumbuzi kwa manufaa ya pande zote mbili za Muungano.

Ameziagiza Wizara za Fedha na Mipango za SMT na SMZ kuchukua jitihada za makusudi kuzitafutia ufumbuzi hoja zinazohusu ushirikiano katika masuala ya fedha ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi.

Aidha, Makamu wa Rais amesisitiza sekta zote kuendeleza vikao vya kisekta kwa pande zote mbili za Muungano ili kupunguza hoja zinazoletwa kwenye kamati ya Pamoja.

Kwa Upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amemhakikishia Makamu wa Rais kwamba ofisi yake itaendelea kuratibu vizuri na kwa weledi mkubwa katika kutatua kero mbalimbali zinajitokeza kwa wananchi katika masuala ya muungano.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Abdullah amesema kusainiwa kwa hati hizo kutaondosha migongano kwa vizazi vya sasa na baadae pamoja na kuwaleta maendeleo wananchi na wawekezaji wa pande zote mbili za jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hapo Awali Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango aliongoza kikao cha kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kushughulikia masuala ya muungano kilichofanyika katika ukumbi wa Idriss Abdul Wakili Zanzibar, kikao kilichopitisha kwa pamoja kuondolewa hoja 11 za muungano zilizopatiwa ufumbuzi.

Settings