Dkt. Mpango akemea viongozi wanaochangia uharibifu wa mazingira

Dec, 19 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Philip Mpango amewataka baadhi ya viongozi wanaochangia katika uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji kuacha mara moja ili kunusuru Taifa dhidi ya athari za uharibifu zinazojitokeza hivi sasa.

Makamu wa Rais amesema hay oleo tarehe 19 Desemba 2022 wakati akifungua Kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji linalofanyika katika Ukumbi wa Masiti mkoani Iringa. Amesema ni vemaviongozi kuachana na maslahi binafsi ili kunusuru mito yote kwani madhara kwa jamii ya watanzania ni makubwa zaidi.Makamu wa Rais amesemani lazima kushirikiana na kuwa na jitihada za pamoja baina ya serikali, dini, sekta binafsi, vyombo vya Habaripamoja na vyama vya siasa katika kupambana na uharibifu wa Mazingira nchini.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewaasa Waandishi wa Habari kuendelea kutumia ushawishi walionao katika jamii kuihamasisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira na kuziagiza taasisi za Serikali kuhakikisha zinawashirikisha Waandishi wa Habari na Vyama mbalimbali vya Wanahabari vinavyojitoa kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira.Pia amewasihi wahariri na waandishi kuandika habari na taarifa za kuelimisha umma za kiuchunguzi na kuepukana na kuandika habari bila kufanya tafiti za kutosha au kujiridhisha hivyo kupelekea habari za upotoshaji hapa nchini.

Makamu wa Rais amewaasa wahariri na wanahabari wote kwa ujumla kuwa wazalendo na kulinda taswira na maslahi ya nchi kwa kuepuka kuwa mstari wa mbele katika kutetea mambo yanayohujumu taifa. Amewatakakujiepusha nakupokea fedha, mali au vishawishi vingine kutoka kwa watu wachache wenye jeuri ya pesa au madaraka ili kupindisha ukweliwa mambo kinyume na maslahi ya taifa au wananchi wengi wanyonge wasio na sauti.

Pia ametoa wito kwa wanahabari wito kusaidia kuelimisha jamii kuhusu fursa zitokanazo na utunzaji wa mazingira ikiwemo biashara ya Kaboni, inayofanyika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani hususan, kwa kupunguza gesijoto. Amesema biashara hiyo ni fursa ambayo itachangia katika pato la Taifa na kuimarisha suala zima la uhifadhi wa mazingira.

Makamu wa Rais amewasihi kutumia Kongamano hilo kufanyamijadala ya kinaya kujenga na kupata maazimio ambayo pamoja na mambo mengine, yatajumuisha hatua mbalimbali zitakazochukuliwa katika kuongeza juhudi za kuhabarisha umma kuhusu utunzaji na ulinzi wa mazingira hususan katika Vyanzo vya Maji.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Kituo cha WanahabariWatetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA) amesema wanahabari watetezi wa rasilimali kwa umoja wao watahakikisha wanashiriki katika mapambano ya kuhakikisha wanalinda na kuhifadhi na kutetea rasilimali za nchi ikiwemo suala la mazingira. Aidha ametoa wito kwa mamlaka za usimamizi kuwasimamia watendaji waliopewa dhamana ya ulinzi wa vyanzo vya maji ili waweze kutimiza wajibu wao na kuepukana na athari za uharibifu zinazojitokeza hivi sasa.

Wanahabari hao watetezi wa Rasilimali wamesema wameshuhudia mto Ruaha ukifikisha siku 130 bila kutiririsha maji licha ya maji hayo kuwepo katika chanzo cha mto ambao huzuiliwa na baadhi ya wananchi wachache wanaofanya shughuli mbalimbali za kilimo jirani na mto huo.

Kongamano hilo linaratibiwa na Kituo cha WanahabariWatetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA) kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri nchini na linashirikisha wanahabari, wadau wa mazingira, viongozi wa serikali, dini, vyama vya siasa pamoja na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Settings