Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali inatarajia kufanya tathmini katika maeneo mbalimbali nchini kubaini athari za mafuriko zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema hayo wakati akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali katika kikao cha kuwasilisha taarifa ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira iliyotokana na mvua za El Nino kwa mwaka 2023/24 na namna Ofisi ilivyokabiliana nazo.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma leo Agosti 13, 2024, Dkt. Kijaji amesema tayari Ofisi ya Makamu wa Rais imeanza kuandaa maandiko kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
“Tutatumia wataalamu waliobobea katika eneo la utafiti ili kueleza umma wa Watanzania kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na namna Serikali inavyochukua hatua kukabiliana nazo,“ amesema.
Aidha, Mhe. Dkt. Kijaji amesema hatua zinazochukuliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau ni kutoa taarifa kwa wananchi hasa wa ngazi za vijiji na kata kuhusu madhara ya mvua za El Nino pamoja kuwa na mpango maalumu wa hatua za awali na mkakati wa kuchukua hatua za dharura hasa kwenye maeneo yanayoathirika mara kwa mara na mafuriko.
Halikadhalika, amesema Serikali inaendelea kuzuia shughuli za binadamu ndani ya mita 60 katika vyanzo vya maji kupunguza idadi ya wananchi na mali za kudumu zinazoathiriwa na matukio yanayotokana na
Mvua.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema Ofisi ipo katika mpango wa kuandaa kitabu ambacho kinaeleza namna ya matumizi ya rasilimali katika fukwe za maji.
Pia, amesema umeandaliwa mfumo wa kitaasisi wa utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu pamoja na kuendelea kutoa elimu zaidi ili wananchi waweza kupata uelewa mpana.
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga kutokana na masuala ya mabadiliko ya tabianchi kuwa endelevu, alitoa wito kuwepo na vituo vya kiutafiti kwa ajili ya kufanya tathmini na kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi.
Taarifa hiyo inalenga kutoa taswira kuhusu namna mazingira yalivyoathirika kutokana na mvua zilizonyesha kati ya Mwezi Novemba, 2023 hadi Mwezi Aprili 2024 na hatua zilizochukuliwa za kukabiliana na hatua hizo.
Tathmini ya athari za mvua za El Nino iyofanyika imehusisha maeneo ya Ukanda wa mashariki katika wilaya za Rufiji, Kibiti, Kisarawe, Kinondoni, Temeke, Kigamboni na Mlimba, ukanda wa Kaskazini katika Mkoa wa Arusha ni Kata ya Kisongo, Wilaya ya Arumeru, Kata za Suye na Mianzini (Jiji la Arusha), Mto wa Mbu (Wilaya ya Monduli), Ngara Mtoni (Halmashauri ya Wilaya ya Arusha-Wilaya ya Arumeru) na Wilaya ya Karatu.
Pia, katika Ukanda wa Magharibi (mikoa ya Kigoma na Katavi) na Nyanda za Juu Kusini (Mikoa ya Rukwa, Mbeya, Njombe na Songwe) ulihusika katika tathmini hiyo.