​Dkt. Jafo: Miradi yote kutekelezwa kwa ufanisi

Jan, 04 2022

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimedhamiria kuhakikisha miradi ya maendeleo kupitia Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo inatekelezwa kwa ufanisi.

Dkt. Jafo ametoa kauli hiyo Januari 4, 2022 wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua na kuzindua miradi ya maji safi na salama katika majimbo ya Chumbuni na Amani pamoja ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Skuli ya Msingi Sebleni jimbo la Kwahani yaliyopo Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi, inayotekelezwa kupitia Fedha za Kuchochea Maendeleo ya Jimbo (CDCF), Zanzibar.

Akizungumza kwa nyakati tofauti akiwa kwenye ziara hiyo alisema kuwa kupitia usimamizi thabiti wa watendaji Serikali zote mbili zitahakikisha miradi hiyo inakamilika kwa viwango na ufanisi mkubwa.

Pia waziri huyo aliwapongeza wataalamu wanaosimamia miradi hiyo kwa kusema kuwa anafarijika kuona matumizi ya fedha yanaendana na ubora na viwango.

“Leo hii hata ukisema miradi haitekelezeki, mimi nasema hapana maana Nimefika hapa nimejionea mwenyewe miradi hii iko vizuri naomba niwapongeze sana kwa kuisimamia vyema na kuitekeleza kwa wakati,” alisema.

Aidha, Waziri Jafo aliongeza kwa kusema kuwa Kukamilika kwa miradi ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo kutatoa fursa na kuwanufaisha wananchi pamoja na kubadilisha maisha yao kwa ujumla.

Kwa awali akizungumza katika mkutano huo na wananchi wa Shehia ya Banko katika Wilaya ya Magharibi Rashid Simai Msaraka alisema aliahidi kuwa wataendelea kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo zinatumika kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Amani, Mhe. Mussa Hassan Mussa alipongeza juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo huku akiwataka kutoiharibu ili iendelee kuwanufaisha.

Awali Dkt. Jafo alishiriki uzinduzi wa gati ya Bandari ya Mkokotoni iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja uliofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi, ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Settings