Dkt. Jafo: Karibuni tuchape kazi

Jan, 10 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo amesema Ofisi yake imefanikiwa kutatua changamoto za Muungano11 kati ya 18 zizokuwa zimesalia ndani ya kipindi kifupi na lengo ni kuongeza kasi katika kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizosalia.

Dkt Jafo ameyasema hayo leo Januari 10, 2022 wakati wa hafla fupi ya kuwakarisha viongozi walioteuliwa kuongoza Ofisi ya Makamu wa Rais na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni wakiwemo Naibu Waziri Mhe. Khamis Khamis na Naibu Katibu Mkuu – Muungano Bw. Abdallah Mitawi.

“Mwaka 2006 ilianzishwa Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya Muungano, kikao ambacho huhusisha Makatibu Wakuu na Mawaziri wa pande zote za Muungano na kuongozwa na Mhe. Makamu wa Rais, kikao hiki ni muhimu sana katika kuzipatia ufumbuzi changamoto za Muungano” Jafo alisisitiza.

Amesema kwa upande wa Mazingira Ofisi yake imefanya marekebisho ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 ambayo imejumuisha masuala mtambuka ambayo hayakuwepo kwenye Sera ya Mwaka 1997 na kutolea mfano wa masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi.

“Sera ya Mazingira ya mwaka 1997 ilipelekea kutungwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake ambazo ni msingi katika usimamizi wa Mazingira nchini” Jafo alifafanua.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis H. Khamis na Naibu Katibu Mkuu – Muungano kwa pamoja wameahidi kufanya kazi kwa bidii katika kuendeleza agenda ya maendeleo endelevu, katika kuimarisha Muungano na kusimamia mazingira kikamilifu.

Settings