Dkt. Jafo: Bajeti imezingatia hifadhi ya mazingira

Jun, 29 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 imezingatia hifadhi ya mazingira.

Amesema hayo mara baada ya kuahirishwa kwa Mkutano wa 11 wa Bunge wakati akitoa tathmini kuhusu hotuba ya bajeti hiyo iliwasilishwa na Serikali hivi karibuni.

Dkt. Jafo amepongeza kwa kusema kuwa bajeti imegusa wizara za kisekta kwa upande wa mazingira kwasababu zimetengewa bajeti inayotosha kutekeleza miradi ya kimazingira.

Amesema bajeti imetenda haki kwa upande wa mazingira kwani Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ndiyo inayoratibu sekta hii imetengewa fedha kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uhifadhi wa mazingira.

Waziri Jafo amesema ana imani kwamba katika bajeti ya mwaka huu kwa kiwango kikubwa Tanzania imetoa mchango mkubwa duniani katika suala zima la kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Akitolea mfano Wizara ya Kilimo amesema kuwa imetengewa bajeti kubwa kwa ajili ya utengenezaji wa mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji hususan katika maeneo yaliyoathirika na changamoto hiyo.

Hali kadhalika Waziri Jafo amesema kuwa bajeti imeinufaisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo imetengewa kiasi cha fedha kwa ajili ya uchimbaji wa malambo ya kunyweshea mifugo hasa katika maeneo kame.

Kwa upande mwingine amebainisha kuwa miradi ya kimkakati ikiwemo ya Bwawa la la kufua umeme la Mwalimu Nyerere pamoja na nishati jadidifu imetengewa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake ambayo itasaidia kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayoendelea kujengwa itakwenda kutumia nishati ya umeme badala ya mafuta hivyo kupunguza uchafuzi wa mazingira unaotokana na moshi.

Hivi karibuni Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba aliwasilisha Bajeti ya shilingi trilioni 44.38 ambayo tayari imepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji.

Settings