Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameielekeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kufanya ukaguzi wa mfumo wa maji ya mvua ili kubaini waliounganisha mfumo wa majitaka kwenye mfumo huo.
Ametoa kauli hiyo leo alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua usafi wa mazingira katika Soko la Kimataifa la Samaki Feri jijini humo pamoja na fukwe za bahari jijini humo.
Dkt. Jafo alisema kuna baadhi ya wananchi wameunganisha mfumo wa majitaka kwenye mfumo wa maji ya mvua unaopeleka maji baharini hali inayohatarisha usalama wa maisha ya wanadamu na viumbe hai hivyo wachukuliwe hatua za kisheria.
Pia, alilitaka jiji hilo kuwatumia maafisa mazingira kupitia upya mifumo ya maji hya mvu na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuondoa kero ya maji hayo kuchanganyika na majitaka.
Aliitaka Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha uhifadhi na utunzaji wa mazingira unazingatiwa ipasavyo.
Katika hatua nyingine waziri huyo alitoa mwezi mmoja kwa jiji hilo kuhakikisha mchanga uliopo pembezoni mwa ufukwe kwani umekuwa ukizuia maji ya mvua kwenda baharini hali inayosababisha madimbiwi ya majitaka.