Dkt. Jafo ataka taasisi za mazingira ziungwe mkono

Jul, 31 2022

Jamii imetakiwa kuziunga mkono taasisi zinazojishughulisha na shughuli za mazingira ili ziweze kufanikisha azma ya Serikali ya kuhakikisha hifadhi na utunzaji wa mazingira unaimarika.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo wakati akizindua Taasisi ya Ealvine Walingozi (EWF).

Alisema mazingira ni muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu hivyo taasisi zinazojishughulisha na masuala ya mazingira ziungwe mkono ili ziweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za utunzaji mazingira.

“Ndugu zangu uchumi wetu unategemea agenda ya mazingira kwa mfano miradi mbalimbali inayotekelezwa inategemea mazingira na hata kilimo kinategemea mazingira ili tuweze kufanikiwa kulima mazao kwa hiyo tuziunge mkono taasisi hizi na ipongeza taasisi hii kwa kushiriki katika kutunza mazingira” alisema.

Pia, Waziri Jafo alizipongeza taasisi za elimu zikiwemo shule za msingi na sekondari kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za upandaji miti kupitia ‘Kampeni ya Soma na Mti’ ambayo mwitikio wake ni mkubwa.

Kwa upande wake Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Prof. Davis Mwamfupe alimpongeza Waziri Jafo kwa kuwa mstari wa mbele kusimamia vyema mazingira ikiwemo kampeni ya kuikijanisha Dodoma.

Alisema zinaonekana jitihada kubwa zikifanyika kuhakikisha nchi yetu inakuwa ya kijani na kuwa haitakuwa jambo jema kuimba wimbo wa ‘Tanzania ni nchi ya furaha’ wakati maeneo katika mengine kunafanyika uharibifu wa mazingira.

Settings