Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu
amesema miradi ya reli ya kisasa (SGR), mradi wa kufua umeme wa Mto Rufiji na
mabasi ya mwendo kasi (DART) ni jitihada za Serikali katika kupambana na athari
za hewa ya ukaa.
Zungu alisema hayo leo wakati alipotembelea Kituo cha Taifa
cha Ufuatiliaji Hewa ya Ukaa (NCMC) kilichopo katika Chuo cha Kilimo (SUA)
mjini Morogoro ambapo alikipongeza na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto zake.
Alisema pamoja na jitihada hizo za Serikali za kupambana na
hewa ya ukaa lakini pia alitoa rai kwa wananchi kutumia nishati mbadala,
kupanda miti ambayo kwa namna moja inasaidia katika kupunguza hewa ya ukaa.
Akifafanua zaidi waziri huyo alitahdharisha kuwa hewa ya
ukaa inaeweza kuwa na athari kubwa kwa vizazi vijavyo kama hatutaamua kuchukua
hatua katika kupambana na changamoto hiyo.
Alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali lakini pia
alitoa mwito kwa wananchi ambao ni wadau wakubwa wa mazingira ili watoe mchango
wao na kushirikiana na Serikali katika kuondokana changamoto hiyo.
“Tunataka sasa wananchi wajue madhara ya kulima kwenye
vyanzo vya maji na athari ya hewa ukaa inatokana na shughuli za kibinadamu hasa
ukataji wa miti na tumesikia taarifa hapa ya namna miti inavyopotea kuanzia
mwaka 2002 hadi mwaka 2013 miti takriban 464,000 imepotea hii ni hatari kwani
inaweza kusababisha nchi kuelekea kuwa jangwa,” alisema.
Akipingeza NCMC kwa kazi nzuri wanayofanya waziri huyo
aliwaomba wakamilishe taratibu ili waweze kupata fedha kutoka Hazina ambazo
zitasaidia kukifanya kituo kiwe chini hya SUA badala ya kutegemea wafadhili
kutoka nje.
Awali akiwasilisha mada Mratibu wa kituo hicho, Profesa
Eliakimu Zabibu alisema Tanzania ambayo ni nchi mwanachama wa Mkataba wa
Umoja wa Mataifa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) inaweza
kufaidika na sera kama Mpango wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa Ukaa kutokana na
ukataji miti ovyo na uharibifu wa Misitu’ – MKUHUMI (REDD+).
Profesa Zabibu alisema faida za MKUHUMI ni kuimarisha
utunzaji misitu nchini,kupata fedha kutoka vyanzo mbalimbali.
Ili nchi iweze kushiriki katika shughuli za MKUHUMI ni
sharti ikamilishe vigezo vya kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Upunguzaji wa Hewa
Ukaa pamoja na Mpango kazi, kuandaa Takwimu za Msingi za Kiwango Rejea cha Hewa
Ukaa kinachozalishwa kutokana na upotevu na uharibifu wa
misitu nchini (Forest Reference Emission Level- FREL); Kuanzisha mfumo
madhubuti wa Upimaji, Uwasilishaji na Uhakiki wa Kaboni (Measurement, Reporting
and Verification- MRV System);
Kuweka mfumo wa Kinga za Athari zinazoweza kutokea kutokana
na utekelezaji wa shughuli za MKUHUMI (REDD+Safeguard System); na Kuandaa mfumo
wa Wazi na Thabiti wa Malipo yatokanayo na utekelezaji wa MKUHUMI.