Ummy awaahidi wanawake utoaji vibali vya mazingira wa haraka

Mar, 09 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Ummy Mwalimu amewaahidi wanawake kuwa atahakikisha anatoa kipaumbele kwenye kutoa vibali vya mazingira kwa biashara au uwekezaji unafanywa na mwanamke.

Pia ameahidi kuanzisha dirisha maalumu la kuwasaidia wanawake katika uwekezaji ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanapotaka kuwekeza.

Ummy alisema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji Tuzo za Viwanda kwa Wanawake Wajasiriamali Tanzania iliyoandaliwa na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (Tanzania Women Chamber of Commerce) kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

"Nawaahidi kupitia NEMC (Baraza la Taigfa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira) nitaanzisha dirisha maalumu la biashara na uwekezaji ili kuweka mazingira mazuri kwa mwanamke anayetaka kuwekeza awekeze bila vikwazo, moja ya vipaumbele ni kuhusu vibali kutoka kwa wakati," alisema.

Waziri huyo aliwataka wanamke kutokata tamaa, wajitume na kuondoa uoga kwamba jamii itawachukulia kwa mtazamo tofauti atakapowekeza au kufanya biashara fulani. Hii itamsaidia kufikia malengo aliyojiwekea yatimie kwa mafanikio makubwa.

"Ndugu zetu wanaume hawaogopi ndiyo maana wapo mbali katika kufanya biashara na uwekezaji kwahiyo nasisitiza kuwa mwanamke aondoe hofu anapotaka kuwekeza, afanye kazi kwa bidii ili aweze kufikia malengo na mafanikio makubwa katika uwekezaji," alisema.

Aidha, Waziri Ummy aliwaomba wanawake washirikiane, wasaidiane wawe na umoja hususan linapokuja suala la biashara na uwekezaji kwa wanawake.

"Nimeona kuna majukwaa mengi ya wanawake yanayohusu biashara na uwekezaji, lakini ningependa liwepo jukwaa moja la biashara, viwanda na uwekezaji linalowaunganisha wanawake," aliongeza.

Aidha Mhe. Ummy alitoa rai kwa wanawake kuchangamkia fursa kwenye sekta ya mazingira, mfano kupitia marufuku ya mifuko ya plastiki watengeneze mifuko mbadala. Pia watumie nishati mbadala wakati wa uzalishaji kuliko kutumia nishati ya miti, hii itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira na kuzuia mabadiliko ya tabianchi.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Watoto, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mwajuma Magwiza, amesema kupitia mamlaka za Serikali za Mitaa, Serikali imekuwa ikitenga fedha za mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake kupitia vikundi ili kuwapa fursa ya kuanzisha biashara na uwekezaji.

Akiongea katika hafla hiyo, Rais wa wanawake wajasiriamali Tanzania, Maida Waziri,amesema adui wa mwanamke siyo mwanamke bali ni umasikini, wanawake washirikiane kuukataa umasikini kwa vitendo kupitia upendo, kusaidiana na kushirikiana katika biashara na uwekezaji kwenye vyama vyote vya wanawake ili viwe na nguvu katika kutatua matatizo au changamoto zinazowakabili wanawake.

"Natoa rai kwa vyama vyote vya wanawake wajasiriamali viungane ili viwe na umoja wenye nguvu ya kuyasemea matatizo yao kwenye vyombo vya Serikali na kupatiwa ufumbuzi kwa urahisi."

Settings