Waziri Ummy: Waingizaji zebaki mkajisajili, Serikali haijapiga marufuku

Mar, 05 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Ummy Mwalimu amewataka waingizaji na watumiaji wa kemikali aina ya zebaki kujisajili kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Pia amesema kuwa Serikali haijazuia uingizaji na utumiaji wa kemikali hiyo hususan kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu.

Waziri Ummy alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na wachimbaji wadogo eneo la Nholi wilayani Bahi mkoani Dodoma alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za uhifadhi mazingira katika migodi.

Alisema kuwa asilimia 80 ya kila kilo 100 za zebaki zinazoingizwa nchini hutumika katika shughuli za uchenjuaji hivyo Serikali inawajibika kupunguza matumizi ya kemikali hiyo ifikapo mwaka 2025.

“Ndugu zangu napenda kusisitiza zebaki si haramu na si madawa ya kulevya na wala si bangi hivyo wanaoingiza au kusambaza msijfiche hamtakamatwa. Sisi Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Madini tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha tunapata teknolojia mbadala ya kuchenjua dhahabu rahisi na isiyo na madhara,” alisema.

Aidha waziri huyo alisema ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imebainisha zebaki ni moja ya madini hatari zaidi na kuwa inahatarisha afya ya binadamu kwani inaweza kusababisha magonjwa ya saratani na figo pamoja madhara kwa wanyama na mimea.

Kwa upande mwingine aliwataka wachimbaji hao kutunza mazingira yanayozunguka migodi yao kwa kutokata miti ovyo ili kutumia katika shughiuli za uchimbaji na badala yake wapate vibali vya kuitumia miti hiyo.

Pia aliwataka waache kuchimba mashimo ovyo wakati wa kutafuta maeneo yenye dhahabu na badala yake wayafukie pamoja na kuhakikisha zebaki haisambai ovyo kwani inaweza kuleta madhara.

Waziri Ummy alisema Serikali inawatambua wachimbaji wadogo kwa kuwa wananajipatia kipato kutokana na shughuli hizo na pia wanaipatia Serikali mapato.

Aliwataka wamiliki wa migodi kuwapatia vifaa vya kujikingia wafanyakazi wao ili kuepuka madhara ya zebaki na kuahidi kujengwa kwa kituo cha umahiri wa uchimbaji ili wachimbaji wa eneo hilo wajifunze.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda alisema wilaya yake inatekeleza agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Samia Suluhu Hassan la kupanda miti milioni moja kila wilaya.

Alisema kuwa ameelekeza kila kata wilayani kwake kupanda miti 50,000 na kuendelea na pamoja na kuzitaka kila kaya kupanda miti isiyopungua mitano na kuitunza hatua inayosaidia katika utunzaji wa mazingira.

Aidha Munkunda alimuomba Waziri Ummy atoe mwongozo kuhusu uchimbaji unafanyika kiholelea katika kingo za mito na kusababisha kutanuka hivyo kupata changamoto ya mafuriko kila mara.

Pia alisema kuna changamoto katika eneo la wachimbaji wadogo wanajichimbia ovyo mashimo na kuyaacha bila kuyafukia kwa kuwa hawana uwezo wa kufanya utafiti wa kubaini miamba yenye madini.

Itakumbukwa Tanzania ilisaini Mkataba wa Minamata kuhusu zebaki Oktoba 10, 2013 na madhumuni yake ni kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya madhara yanayotokana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na zebaki.

Madhumuni mengine ni pamoja na kulinda vyanzo vya uchafuzi katika maeneo ambayo kemikali hiyo ya zebaki inatumiwa kwa kudhamiria au kujitokeza kwa kutodhamiria huku.

Zebaki inatajwa kuleta athari kwa binadamu hususan katika mfumo wa neva za fahamu, kusikia, kuongea, kuona, kumeng’enya na kumeza chakula na pia huathiri viungo muhimu kama moyo, mapafu, ini, figo na hata mimba.

Settings