Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka halmashauri zote nchini zihakikishe kuwa zinaweka vituo vya kuchakata na kutenganisha taka ili zinapozalishwa ziweze kushughulikiwa kwa njia salama na endelevu, kwa lengo la kupunguza mzigo wa taka unaokwenda majalalani au kusambaa ovyo katika makazi ya watu.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa zishirikiane na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kuandaa mipango ya kuwezesha jamii na vijana kushiriki biashara ya kaboni, kutumia na kuendeleza teknolojia za nishati safi na miradi ya urejelezaji wa taka (recycling).
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Juni 03, 2025 alipozungumza na vijana katika Jukwaa la Vijana na Mazingira lililofanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo hufanyika Juni 5 kila mwaka ambapo kitaifa yatafanyika Jijini Dodoma.