Waziri Masauni: Tanzania imenufaika na fedha za mabadiliko ya tabianchi
Jun, 18 2025
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Serikali ya Tanzania imenufaika kwa kiasi kikubwa na fedha za miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kufuatia jitihada na ushawishi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika majukwaa ya kimataifa.
Akizungumza mbele ya wananchi wa Bariadi Juni 18, 2025 wakati wa mkutano wa hadhara wa majumuisho ya ziara ya Rais Samia mkoani Simiyu, Mhe. Masauni amesema kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi kama ukame, mafuriko na uharibifu wa uoto wa asili zinatokana na Nchi zinazoendelea.
“Mhe. Rais, moja ya matunda ya juhudi zako ni utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji unaogharimu zaidi ya Euro milioni 313, ambao kesho tutaenda kuutembelea. Huu ni ushahidi kuwa uongozi wako umeleta mageuzi chanya katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Masauni
"Mheshimiwa Rais nipende kukupongeza wewe binafsi tangu ukiwa Makamu wa Rais ulipambana kuhakikisha athari hizi za Mabadiliko ya tabianchi ambayo vyanzo vyake ni nchi zilizoendelea kama nchi yetu tunanufaika na fursa zinazojitokeza.
Pamoja na suala la mazingira Waziri Masauni amezungumzia matunda ya Muungano ambapo ameeleza watu wengi wa bara wanaishi Zanzibar kama ilivyo kwa watu wa Zanznibar ambao huishi Bara.
“Watu wenye asili ya usukuma wapo Zanzibar na watu wenye asili ya Zanzibar wapo Simiyu.”