Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo amezipongeza taasisi na mashirika ya dini kwa juhudi kubwa inazoendelea kufanya katika kuhamasisha na kuunga mkono ajenda ya mazingira inapewa kipaumbele katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Dkt. Jafo ameyasema hayo leo Ijumaa (Juni 23, 2023) wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) katika hafla iliyofanyika katika Dayosisi ya Dodoma na kuongozwa na zoezi la upandaji miti 1,000 katika Dayosisi hiyo.
Waziri Jafo amesema Dayosisi ya KKKT Dodoma imetoa mfano halisi wa ushirikiano unaopaswa kupigiwa mfano baina ya serikali na taasisi za dini ambapo kwa kutambua umuhimu huo Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira ili kuratibu vyema masuala ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
Dkt. Jafo amesema kwa mujibu wa malengo ya ilani ibara ya 68 kifungu L ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM 2020-2025 Mkoa ulipewa malengo ya kupanda miti Milioni 40,000 ikilinganisha na Mikoa mingine ambapo Halmashauri zao zimeelekezwa kupanda miti Milioni 1,500,000 na kuipongeza Dayosisi ya Dodoma kwa kutekeleza kwa vitendo malengo hayo ya ilani.
Aidha Dkt. Jafo amesema Serikali kupitia taasisi zake ikiwemo Wakala wa Huduma za MisItu Tanzania (TFS) itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wadau mbalimbali kwa kutoa miti yenye mazingira rafiki kwa kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa ajenda na dhamira ya Serikali ya uhamasishaji wa mazingira inafikia malengo yake.
“Nimesikia katika taarifa yenu namna mnavyoshirikiana na TFS namna mnavyopanda miti katika maeneo yetu, nawaombeni sasa juhudi kubwa mzielekeze katika kustawisha vitalu na kugawa miti katika maeneo yote ya Tanzania kwa lengo la kuhakikisha kuwa tunapambana na uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi” amesema Dkt. Jafo
Akifafanua zaidi kuhusu athari za uharibifu wa mazingira, Dkt. Jafo amesema kwa sasa dunia inakabiliwa na changamoto ya ongezeko ya kiwango kikubwa cha joto ambapo tangu mwaka 2015 Mataifa mbalimbali yakitakiwa kupunguza kiwango cha joto kwa kuzingatia Mkataba wa Paris kwa angalau digriii 1.5.
Amesema kutokana na ongezeko hilo la joto duniani, baadhi ya mataifa yameanza kushuhudia kuongeza kwa maji ya bahari hatua inayotokana na kupasuka kwa vipande vya barafu maeneo ya bahari na kufanya kina cha bahari kuongezeka na hivyo kuleta athari kubwa kwa ustawi wa viumbe hai wa majini na nchi kavu.
Waziri Jafo ametaja changamoto nyingine ya uharabifu wa mazingira ni pamoja na kuongezeka kwa hali ya ukame hatua inayofanya upatikanaji wa maji kuwa hafifu na kutotosheleza kwa mahitaji yake kwa matumizi ya wanyama, binadamu na mimea na hali hiyo inajidhihirisha katika sekta uzalishaji mali ikiwemo kilimo.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Anna Lupembe amelipongeza KKKT ameipongeza Kanisa la KKKT Dayosisi ya Dodoma kwa kutambua dhamira na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kusimamia masuala ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
“Viongozi wetu Wakuu, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango wanahimiza suala la uhifadhi wa mazingira. Naipongeza Dayosisi kwa juhudi hizi kwani nchi yetuilishapoteza uoto wa asili lakini tunashuhudia taasisi mbalimbali zinajitokeza kwa ajili ya kurejesha uhalisia wa mazingira ya nchi yetu na dunia kwa ujumla” amesema Lupembe.
Aidha Mhe. Lupembe ametoa wito kwa Dayosisi hiyo kutenga maeneo maalum ya kupanda miti kwani sasa mti una thamani kubwa kiuchumi ikiwemo biashara ya kaboni na hivyo kuitaka Dayosisi na majimbo ya kanisa hilo hiyo kuhimiza jamii ili ipate kuchangamkia biashara hiyo.
Naye Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T) Dayosisi ya Dodoma Askofu Christian Ndossa amesema kanisa mbali na huduma za kiroho kanisa hilo pia limekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha suala la utunzaji na usimamizi wa mazingira, kutoa elimu ya mazingira kwa kuwa ni agizo la mungu linalohimiza jamii kuishi katika mazingira salama.
“Leo tumekutana katika kutekeleza vipaumbele vya Serikali vya kuhifadhi Mazingira kwa kupanda miti. Ajenda hii ni mojawapo ya vipaumbele muhimu vya Dayosisi yetu na tumetoa msisitizo mkubwa kwa kutambua kuwa Mkoa wa Dodoma ni moja ya Mikoa inayoathriwa na ukame na shughuli kuu ya kiuchumi ni kilimo, hivyo tutaendelea kuhamasisha jamii kupanda miti” amesema Askofu Ndossa..
Aidha amesema katika kuhimiza kampeni za upandaji miti katika majimbo na masharika, Dayosisi hiyo imekusudia kupanda miti 30,000 ambapo wameanza na miti 1000 katika Dayosisi ya Dodoma ambapo ameishukuru Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kwa kuendelea kuiunga mkono Dayosisi kwa kuipatia miche ya miti.
Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba amesema Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kutoa ushirikiano kwa miaka zaidi kwa kutoa miaka miongozo na upatikanaji wa miti ya aina mbalimbali inayoweza kumudu hali ya hewa kuliungana na maeneo inapopandwa.
“Ofisi ya Makamu wa Rais inaipongeza Dayosisi.kuadhimisha miaka 60 kwa kufanya shughuli mbalimbali za uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti kwani kitendo hicho ni kiashiria cha mwitikio wa taasisi na mashirika zisizo za kiserikali kuunga mkono juhudi za serikali” amesema Dkt. Komba.