Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo amekutana na wadau wanaojishughulisha na shughuli za taka hatarishi jijini Dar es Salaam ambapo amesema hivi karibuni kumejitokeza changamoto nyingi katika kusimamia jukumu hilo.
Jafo alisema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau ilifanya mapitio na kufanya marekebisho ya Kanuni za Udhibiti wa Taka Hatarishi za Mwaka 2019 na kuandaa Kanuni mpya za Udhibiti na Usimamizi wa Taka Hatarishi za Mwaka, 2021 (The Environmental Management (Hazardous Waste Control and Management), 2019 na kufanya mapitio ya Kanuni za Ada na Tozo za Mwaka, 2019 na kuandaa Kanuni za Ada na Tozo za Mwaka, 2021.
Waziri huyo alibainisha kuwa pamoja na masuala mengine, lengo kuu la kufanya mapitio ya Kanuni hizi lilikuwa ni kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa taka hatarishi nchini.
"Ikiwa ni takriban miezi miwili sasa tangu Kanuni hizi zilipopitishwa mwezi Mei, 2021 na kuanza utekelezaji wake, nimeona ni vyema pia tukumbushane matakwa ya Kanuni hizi na nyie wadau mtueleze changamoto mnazokumbana nazo katika kuzingatia matakwa ya Kanuni husika ili sote kwa pamoja tuweze kuimarisha usimamizi wa taka hizi," alisema.
Aidha, Jafo aliwakumbusha wadau hao kuwa Tanzania imeridhia Mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo inatoa fursa ya ushirikiano wa kimataifa katika kusimamia na kudhibiti usafirishaji wa taka hatarishi baina ya nchi na nchi.
Aliitaja baadhi ya Mikataba hiyo ni Mkataba wa Basel unaosimamia udhibiti wa usafirishaji wa taka hatarishi kutoka nchi moja na kwenda nchi nyingine na Mkataba wa Bamako unaozuia uingizaji na usafirishaji wa taka hatarishi ndani ya Afrika ambayo yote kwa pamoja tuliridhia mnamo mwaka 1993.
Katika kutekeleza matakwa ya Kanuni mpya za Udhibiti na Usimamizi wa Taka Hatarishi za Mwaka, 2021 (The Environmental Management (Hazardous Waste Control and Management), na Utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa tuliyoridhia kumekujitokeza changamoto mbalimbali zikiwemo za baadhi ya wadau kuingiza nchini taka hatarishi bila kupata idhini kutoka Mamlaka za nchi ambayo shehena inatopotoka na inapoingia.
Baadhi ya wadau kuchelewa kuhuisha vibali na hivyo kupelekea usumbufu katika uendeshaji na usimamizi wa shughuli za ukusanyaji, uhifadhi na usafirishaji wa taka hatarishi, baadhi ya wadau kutokuwasilisha taarifa za viwango vya taka hatarishi walivyokusanya/hifadhi/kusafirisha kama inavyoelekezwa katika kanuni za taka hatarishi za mwaka 2021 (Ripoti ya kila nusu mwaka).
Nyingine ni baadhi ya wadau kutowasilisha nyaraka sahihi na kwa wakati na hivyo kusababisha ucheleweshaji katika utoaji wa vibali, pia baadhi ya wadau kutokufuata utaratibu katika kufuatulia vibali vyao ikiwemo kufuatilia vibali moja kwa moja Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira bila kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Changamoto nyingne ni baadhi ya wadau wasio waaminifu kujishughulisha na shughuli za ukusanyaji, uhifadhi na usafirishaji wa Chuma chakavu kuhujumu miundo mbalimbali nchini.
Naye mmoja wa Wafanyabiashara hao kutoka Gaia Industry, Bi. Rehema Ally alitoa maoni kuwa mchakato wa vibali vya taka hayarishi uanze kufanyika mtandaoni (online). Katika suala hilo Waziri Jafo ametoa maagizo kwa NEMC kuwa katika siku 45 mchakato huo wa mtandaoni uwe tayari umekamilika na kuwezesha Wadau kutumia mfumo huo.