Waziri Jafo ashiriki Kongamano kuhusu viwango vya sauti katika nyumba za ibada

Jun, 12 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameshiriki katika Kongamano la Kitaifa la Kujengewa Uelewa Juu ya Athari za Sauti Zilizozidi Viwango katika Nyumba za Ibada lililofanyika leo Juni 12, 2023 jijini Dodoma na kufunguliwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo, lengo ni amesema lengo ni kupeana maelekezo ya kutosha katika upande wa Kanuni na Sheria za Mazingira na kuangalia namna bora na nzuri ya kufanya biashara na ibada ziendelee lakini zikifuata taratibu na sheria za nchi.

Amesema kongamano hilo ni maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyotoa Mei 06, 2023 jijini Dodoma kuwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha inasimamia suala la la kelele na mitetemo katika upande wa taasisi za dini linaratibiwa na Jumuiya ya Marudhioani na Amani

Amesema kuwa pia ni mwendelezo wa utekelezaji wa Sera ya Mazingira ya mwaka 2021 pamoja na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 Sura ya 191 na kanuni zake zikielekeza suala zima la udhibiti wa kelele na mitetemo za mwaka 2015.

Aidha, Dkt. Jafo alisema kuwa kupitia NEMC hivi karibuni imepokea malalamiko 521 ya kelele hali inayoashirikia kuna changamoto kubwa katika jamii ambapo inaathirika kwa kukumbwa na matatizo ya kiafya.

“Kongamano hili limeleta faraja kubwa kwani tunaona makundi mbalimbali yapo hapa kwa ajili ya kupata uelewa wa pamoja katika kudhibiti kelele na tuone namna bora ya kudhibiti changamoto hii,“ alisema.

Aliongeza kuwa Ofisi itakuwa tayari kuhakikisha maelekezo yote ya Serikali yanafanyiwa kazi kwa kuangalia namna bora zaidi kupitia NEMC kufanikisha kila jambo linakwenda kama lilivyopangwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka alisema kuanzia Januari hadi Mei wamepokea zaidi ya taarifa 500 za kelele zinazotokana na nyumba za ibada.

Hivyo, alisema Serikali imeandaa mwongozo na kutoa maelekezo mahususi katika makundi mbalimbali, ikiwemo wanaozalisha sauti zinazozidi viwango kwenye nyumba za ibada.

Kongamano hilo limeandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano Tanzania (JMAT) kwa kushurikiana na NEMC.

Settings