Waziri Jafo ahimiza upandaji miti kwa kila mwananchi kulinda hai

Jan, 25 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema suala la upandaji miti katika maeneo yanayoizunguka jamii ni jukumu la kila mwananchi katika kulinda uhai.

Dkt. Jafo amesema hayo wakati akizindua zoezi la upandaji miti kuelekea Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lililofanyika katika Shule ya Msingi ya Dodoma English Medium leo Januari 25, 2024.

Amesema kwa kutambua Muungano wetu ni tunu ya Taifa letu, na msingi wa maisha ya Watanzania, tumechukua hatua za kuulinda na kuuenzi ikiwa ni pamoja na kuendelea kuelimisha umma kuhusu umuhimu wake katika historia ya Taifa letu.

“Ofisi ya Makamu wa Rais imeona ni vema maadhimisho haya yaende sambamba na shughuli za hifadhi ya mazingira hususani upandaji miti kote nchini. Kila taasisi na wananchi wote katika maeneo yetu wanatakiwa kupanda miti ya kumbukumbu ya miaka 60 ya Muungano,” amesema.

Dkt. Jafo ameongeza kuwa upandaji wa miti kuelekea maadhimisho ya Muungano unafanyika kuendeleza kampeni ya Serikali ya hifadhi ya mazingira hususani, kupanda na kutunza miti na kusema kuwa kama tulivyoungana kulinda uhuru, utamaduni na utaifa wetu, tunahimizwa tuungane kulinda mazinigra yetu.

Aidha, amesisitiza kuwa kila mwananchi anatakiwa kupanda mti wa kumbukumbu ya Muungano na kila taasisi katika ngazi zote, kitaifa, kimkoa na mamlaka za Serikali za Mitaa, inatakiwa kupanda miti isiyopungua 60 kama alama ya miaka 60.

Katika hatua nyingine amehimiza usafi wa mazingira katika maeneo yanayoizunguka jamii ili kujikinga na maradhi ya hususan kipindupindu.

Amezielekeza mamlaka za Serikali za Mitaa kuwasimamia wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la usafi katika mitaa yote ili kuifanya kuwa safi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema mkoa huo umeendelea kutekeleza kampeni ya ‘Soma na Mti’ iliyoasisiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Amesema kuwa wameendelea kusimamia viongozi wa elimu ambao wanatekeleza kampeni hiyo kwa kuhamamsisha kupanda miti wanafunzi wa shule zote za msingi, sekondari na vyuo ili kukijanisha Dodoma.

Mkuu wa Mkoa amesema wameendelea kushirikiana na kampuni za gesi kuhakikisha upatikanaji wa nishati hiyo na kuzisaidia taasisi zinazotumia kuni na mkaa kwa kiwango kikubwa ili kupunguza ukataji wa miti.

Katika zoezi hilo jumla ya miti 60 imepoandwa katika katika eneo la shule hiyo na kutarajiwa kuendelea katika maeneo ya taasisi nyingine za Serikali kwa wiki nzima.

Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kinatarajiwa kufanyika Aprili 26, 2024.

Settings