Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wito kwa wakulima na wafugaji kuendelea kutunza mazingira ili shughuli ziwe endelevu.
Amesema hayo wakati akitembelea mabanda ya Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mjini Morogoro leo Agosti 07, 2023.
Amesisitiza utunzaji mazingira akisema kuwa sehemu kubwa ya kilimo kinategemea mvua na kwamba uharibifu wa mazingira unasababisha athari mbalimbali ikiwemo ukame.
Dkt. Jafo ameongeza kuwa Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kujenga malambo makubwa 114 nchini kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na bila utunzaji wa mazingira kilimo hicho hakitafanikiwa.
“Ndugu zangu tunapokata miti ovyo na kufanya shughuli za kibinadanu kwenye vyanzo vya maji tunasababisha mito yetu kukauka na mito ikikauka kilimo chetu kinachotegemea mvua hakitakuwa na tija, nawaomba tutunze mazingira,” alisisitiza.
Aidha, Waziri Jafo alipongeza waandaaji wa maonesho hayo yanayojumuisha mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Tanga na Pwani maandalizi mazuri ambayo yanatumika kutoa elimu kwa makundi hayo na wananchi kwa ujumla.
Alibainisha kuwa ili kukabiliana na changamoto ya ukame Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua katika uwekezaji kwenye kilimo na mifugo kwa kuhakikusha sekta hizo mbili zinakuwa na tija na manufaa.
Hali kadhalika Waziri Jafo alitoa wito kwa Watanzania kuungana kwa pamoja na kuhakikisha wanalinda rasilimali zilizopo hapa nchini ili ziwe na manufaa kwa jamii nzima.
Kwa upande Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima alisema changamoto ya ukosefu wa mvua inatokana na ukataji miti holela hasa katika maeneo ya milima.
Hivyo, alisisitiza kuwa kila mwananchi mkoani humo ashiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji miti na huku akiwataka wakulima kuacha kulima kwa kuharibu mazingira.
“Miti imekatwa ndio maana kuna changamoto ya athari za mazingira mvua hazinyeshi kwa wakati au hazinyeshi kabisa na kusababisha mtu anashindwa kupanda na akipanda anapata hasara,“ alisema Malima.
Ili kukabiliana na hali hiyo alisema Kanda ya Mashariki wamekuja na mkakati wa kutengeneza ajenda ya kilimo itakayomsaidia mkulima katika kufanya kilimo endelevu na chenye mafanikio.
“Kanda ya Mashariki ina jukumu la kulinda mazingira kutokana na umuhimu wa mito inayopeleka maji katika Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere linalotarajia kuzalisha umeme zaidi ya Megawati 2000,” alisema Malima.