Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha mwaka mmoja leo Machi 2, 2022 jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja cha Serikali Ofisi ya Makamu wa Rais imekamilisha mchakato wa mapitio wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 1997 na kuandaa Sera Mpya ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 ambayo ilizinduliwa Februari 12, 2022 Jijini Dodoma na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
Alisema hiyo imejumuisha masuala ya mazingira yaliyokuwemo katika Sera ya 1997 na masuala mapya ambayo ni pamoja na Udhibiti wa taka za kielektroniki,
Usimamizi na matumizi ya kemikali, Udhibiti wa uchafuzi katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi.
Waziri Jafo alitaja masuala mengine kuwa ni Mabadiliko ya tabianchi, Usimamizi wa matumizi salama ya bioteknolojia ya kisasa na Udhibiti wa viumbe vamizi.
Hivyo, Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 imeongeza wigo wa masuala na changamoto za mazingira zinazopaswa kufanyiwa kazi katika kipindi husika ili kuleta maendeleo endelevu.
Pia, Sera mpya imezingatia changamoto mpya za kimazingira zinazoendelea kujitokeza kutokana na mabadiliko ya mifumo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira yanayoendelea duniani.
Dkt. Jafo alisema kuwa katika kipindi hicho, jumla ya vibali 1445 vimetolewa ikiwemo vibali 1014 vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na vibali 431 vya Ukaguzi wa Mazingira.
Aliongeza kuwa katika Miradi Ya Hifadhi ya Mazingira, Ofisi imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya hifadhi ya mazingira ikiwemo, Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula Katika Maeneo kame ya Tanzania (Reversing Land Degradation and Food Security in Semi-Arid Areas - LDFS).
Mradi huu unatekelezwa katika Halmashauri za Micheweni (Kaskazini Pemba), Magu (Mwanza), Nzega (Tabora), Mkalama (Singida), na Kondoa (Dodoma). Katika kipindi husika, Mradi umetoa hatimiliki ardhi za kimila kwa wananchi 1,448,” alisema.
Kwa upande wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi Kupitia Mifumo Ikolojia (Ecosystem-Based Adaptation for Rural Resilience in Tanzania - EBBAR), ambapo Mradi unatekelezwa katika Halmashauri za Kaskazini A (Unguja), Mpwapwa (Dodoma), Simanjiro (Manyara), Mvomero (Morogoro) na Kishapu (Shinyanga).
Pia Mradi wa majaribio wa Kikanda wa Kukabiliana na Mabailiko ya Tabianchi katika Bonde la Ziwa Victoria (Adapting to Climate Change in Lake Victoria Basin) ambao unatekelezwa na nchi tano (5) ambazo ni Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda na Kenya. Kwa upande wa Tanzania, Mradi unatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mwanza kwa gharama ya Dola za Kimarekani 500,000 sawa na Shilingi bilioni 1.
Kwa upande wa Muungano alisema kuwa vimefanyika vikao vya kujadili masuala ya Muungano katika ngazi mbalimbali ambapo hoja 11 kati ya 18 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.
Dkt. alisema hoja zilizopatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja na Muungano ni pamoja na uingizaji wa maziwa kutoka Zanzibar, Usimamizi wa ukokotoaji na ukusanyaji wa Kodi kwenye Huduma za Simu unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRB).
Alitaja hoja nyingine kuwwa ni Mkataba wa mkopo wa fedha za ujenzi wa Barabara ya Chake chake hadi Wete – Pemba, Mkataba wa mkopo wa fedha za Mradi wa Ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Mkataba wa mkopo wa fedha za ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri, Uvuvi kwenye Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano; Mgawanyo wa mapato yatokanayo na Misaada kutoka Nje ya Nchi, Mapato yanayokusanywa na Uhamiaji kwa upande wa Zanzibar; Uteuzi wa Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Revenue Appeal Tribunal (TRAT) kutoka Zanzibar; na Uteuzi wa Mjumbe wa Bodi ya Bima ya Amana (Deposit Insurance Board - DIB) kutoka Zanzibar.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeendelea kushirikiana katika miradi mbalimbali ya maendeleo na miradi na programu mbalimbali zinazendelea kutekezwa,” alisema.
Waziri huyo alibainisha kuwa miongoni mwa miradi na program ni pamoja na: Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili uliozinduliwa mwezi Februari, 2020 ambapo jumla ya shilingi bilioni 112.9 zitatumika Zanzibar.
“Katika kuimarisha ushirikiano ndani ya miezi kumi na mbili ya Serikali ya Awamu ya Sita (6) vimefanyika vikao 21 na Sekta zilizokutana ni Sekta ya Nishati, Sekta ya Maji, Sekta ya Madini, Sekta ya Uchukuzi, Sekta ya Utumishi na Utawala Bora, Uratibu wa shughuli za Serikali, Sekta ya Viwanda na Biashara, Sekta ya Maliasili na Utalii, Sekta ya Afya, Sekta ya Kilimo, Sekta ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Sekta ya Ardhi, Sekta ya Fedha na Mipango na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.