Wawekezaji waalikwa kutumia fursa ya biashara ya kaboni

Mar, 13 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wito kwa kampuni mbalimbali kutumia fursa ya uwepo wa misitu iliyopo nchini kufanya biashara ya kaboni.

Ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira ilipotembelea Mradi wa Urejeshwaji wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) katika Kijiji cha Ilalasimba, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa mkoani Iringa Machi 13, 2024.

Akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea hifadhi ya msitu wa unaohifadhiwa na wanakijiji cha Ilalasimba, wenye ukubwa wa ekari 5,204, Dkt. Jafo amesema ni wakati muafaka kwa kampuni zaidi ya 30 kuwekeza katika biashara ya kaboni.

Amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais tayari imeandaa mwongozo wa usimamizi wa biashara hiyo kuweka utaratibu na masharti ambayo watazingatia wakati wa utekelezaji, hivyo iwaletee manufaa wananchi wanaotunza misitu kwenye maeneo yao.

Aidha, Waziri Jafo Dkt. Jafo amewaomba wananchi kuitunza misitu na kuacha kukata miti kwa ajili ya matumizi mbalimbali hususan ya kuni na mkaa na badala yake watumie nishati safi ya kupikia.

“Tukumbuke mwezi Oktoba mwaka 2022 Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua kampeni ya nishati safi ya kupikia na alitoa maelekezo, mnakumbuka mwaka jana (2023) Ofisi yetu ambayo ina jukumu la kuandaa miongozo tulitoa tangazo la kutaka taasisi zinazolisha watu zaidi mia waache kutumia kuni na mkaa, zoezi hilo liemekwenda vizuri, hivyo nawaomba Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga amesema kuwa kamati hiyo imeridhika na utekelezaji wa mradi huo hasa katika eneo la uhifadhi wa msitu ambao tayari umeonesha mafanikio kwa kuanza kurejesha uoto wa asili.

Mhe. Kiswaga amesema kuwa kamati inaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika biashara ya kaboni katika maeneo yao kwa kuwahimiza kupanda na kuitunza miti ili iweze kutumika kunyonya hewa ya ukaa.

Halikadhalika, amesema kuwa kupitia ushiriki wa kamati hiyo katika mikutano mbalimbali duniani ukiwemo wa Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika kila mwaka wameendelea kujifunza na kupeleka hamasa kuhusu biashara hiyo katika mataifa mbalimbali.

“Kwa kweli tumeridhishwa na utekelezaji wa mradi huu na tumeona namna unavyosaidia katika kupunguza uharibifu wa mazingira na kupitia msitu huu unaotunzwa tunaziomba kampuni zianze kufanya biashara hii hata kwa kuanza na eneo hili dogo misitu hapa Iringa,” amesisitiza.

Naye Mratibu wa kitaifa wa Mradi wa SLR kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Damas Mapunda biashara ya kaboni imewanufaisha wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ambao Desemba 2023 walipokea mgao wa Sh. bilioni 14.

Dkt. Mapunda amesema kuwa kupitia biashara ya kaboni wananchi walionufaika wameweza kutekeleza shughuli mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya shule na afya.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imetembelea shughuli mbalimbali za mradi zikiwemo hifadhi ya msitu wenye ukubwa wa ekari 5,204,

shamba darasa la mahindi kwa kutumia kilimo cha mzunguko na

wanakikundi cha Agape wanaojishughulisha na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa katika Kijiji cha Ilalasimba.

Mradi wa SLR unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais unatekelezwa ili kuimarisha usimamizi jumuishi wa mazingira na urejeshwaji wa mazingira yaliyoharibiwa ili kujenga uhimilivu wa mifumo ikolojia.

Halmashauri za wilaya zingine zinazonufaika na mradi huo ni Mbeya na Mbarali (Mbeya), Sumbawanga (Rukwa) pamoja na Tanganyika na Mpimbwe (Katavi).

Settings