Watumishi Ofisi ya Makamu wa Rais wapatiwa Mafunzo kuhusu magonjwa yasiyoambukiza

Mar, 23 2024

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Bi. Mary Maganga amesema ni vyema kuwa wazi juu ya kulinda afya zetu sababu itasaidia kupata msaada wa kusaidiwa haraka na kupatiwa matibabu.

Ameyasema hayo wakati wa semina kuhusu magonjwa yasiyoambukiza kwa watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais iliyotolewa na Madaktari pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma Machi 22, 2024.

Bi. Maganga amesema afya njema kwa binadamu ni mtaji katika maisha yake sababu hakuna anayeweza kufanya vyema majukumu yake kama afya yake haiko imara hivyo kila mmoja anatakiwa kuijua afya yake.

“Naamini semina hii itazaa matunda kwetu baada ya kupata elimu juu ya magonjwa mbalimbali katika kulinda afya zetu,” anasema Bi. Maganga.

Naye, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi, Christina Mndeme ameongeza kuwa, kutokana na umuhimu wa elimu iliyotolewa na wataalamu hao ipo haja ya kupanga siku nyingine ili kuweza kusaidia wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kupewa zaidi elimu juu ya afya.

“Naamini hakuna aliyetoka kama alivyoingia, tumejifunza mambo mengi sahivi tumejua chakula kipi kinapaswa kuliwa kwa wakati upi hayo yote baada ya mtaalamu wa Lishe na Chakula kutufundisha lakini tumeweza kujifunza dalili za magongwa mbalimbali na namna ya kujikinga,” amesema Bi. Mndeme.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mafunzo na Utafiti Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Bi. Monica Kessy amesema wafanyakazi wanatakiwa kuwa na utaratibu wa kupima afya zao kila wakati jambo ambalo litawasaida kujua hali ya afya zao.

Aidha, mtaalamu wa chakula na Lishe kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Yasinta Luambano amesema ili kulinda afya ni vyema kupunguza matumizi ya vyakula vilivyoongezwa sukari kama vile soda na juisi za viwandani zilizoongezwa ladha ya matunda.

“Punguzeni ulaji wa vyakula vilivyokaangwa na mafuta mengi, mafuta yenye lehemu nyingi, mafuta yaliyotengenezwa viwandani yenye lehemu nyingi au sukari au chumvi pia nashauri mtu kula matunda badala ya kunywa juisi sababu unapokula matunda inakuwa vyema zaidi kiafya.”

Ameongeza kuwa ni muhimu kuzingatia ulaji unaofaa ilikuzuia na kupunguza magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.

Katika semina hiyo watumishi walifundishwa mambo mbalimbali kama vile kuhusu Ugonjwa wa Saratani, figo, kisukari, Shinikizo la damu, Afya ya Akili pamoja na Lishe.

Settings