Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amewahimiza Watanzania kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake watumie nishati safi ya kupikia ili kuunga mkono jitihada na dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha ifikapo Mwaka 2030 kila mtanzania awe anatumia nishati hiyo.
Amesema hayo aliposhiriki zoezi la usafi katika Mnada wa Nyama Msalato lililoandaliwa na Mabalozi wa Mazingira wa Mkoa wa Dodoma leo tarehe 25 Mei, 2024.
Amesema umefika wakati sasa wa kutumia nishati safi ya kupikia badala ya kutafuta gunia la mkaa ama kuni.
"Mazingira ndio ajenda ya dunia, juzi Mama ametoka Ufaransa alikwenda kushiriki kwenye Mkutano mkubwa wa Kimataifa uliozungumzia masuala ya nishati safi ya kupikia, maana yake tuunge mkono juhudi zake, tukae tujadili tuone namna ambavyo tutaweza kuwatoa wananchi kwenye dhana ya kutumia nishati chafu ile ya kuni na mkaa na kuwaleta kwenye nishati safi ya kupikia,” amesisitiza.
Pia, amewashukuru Mabalozi wa Mazingira wa mkoa huo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuiwakilisha Serikali katika mambo mbalimbali ya utunzaji wa mazingira.
Amesema sio rahisi Serikali kujua kila sehemu yenye changamoto hivyo mabalozi wanafanya jitihada bila ya kulipwa na wanafichua maeneo yenye changamoto.
Amesema Serikali inatambua na kuwashukuru wanapowasilisha changamoto hizo na kuzifanyia kazi.
Mbali na Mabalozi amewashukuru viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na wakazi wa Msalato hususan watumiaji wa Machinjio kwa kuliweka eneo hilo katika mazingira ya usafi