Wataalamu wa Manunuzi wahimizwa kuzingatia miongozo ya ununuzi wa vifaa vyenye ukomo wa matumizi

Aug, 26 2023

Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Serikalini wamehimizwa kuzingatia miongozo ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ili kuepuka manunuzi vifaa vyenye ukomo wa matumizi ambavyo husababisha madhara mbalimbali kwa afya ya binadamu na mazingira.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Juliana Mkalimoto wakati akifunga warsha ya siku mbili ya mafunzo kwa wataalamu hao kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Montreal inayohusu kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni.

Mkalimoto amesema maafisa ununuzi na ugavi ni wadau muhimu wanaopaswa kuzingatia utekelezaji wa itifaki ya Montreal kwa kuwa ndio wahusika wakuu wa huduma ya manunuzi wa vifaa na vitendea kazi mbalimbali vinavyotumika na Serikali kupitia Wizara, Idara na Taasisi za umma katika kutekeleza majukumu yake kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Mkalimoto, Serikali imekuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya huduma za ununuzi na ugavi katika utoaji wa huduma, hivyo ni wajibu wa Maafisa ununuzi na ugavi kuzingatia thamani ya fedha wakati wa kushindanisha zabuni mbalimbali.

“Kama mnavyofahamu Serikali inaendelea na ujenzi wa majengo katika maeneo mbalimbali nchini na mfano mzuri ni kule Mtumba (Dodoma)…Tukiwa kama wataalamu tunapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu wakati wa michakato ya zabuni ili kuepuka uagizaji na uingizaji wa vifaa vyenye ukomo wa matumizi ambavyo vina madhara ya afya kwa binadamu na mazingira,” amesisitiza Mkalimoto.

Aidha, Mkalimoto amesema kwa kutambua umuhimu wa mafunzo hayo kwa watumishi wa kada ya ununuzi na ugavi, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imekusudia kutoa mafunzo hayo kwa maafisa ununuzi na ugavi waliopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekretarieri za Mikoa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Kemilembe Mutasa amesema mafunzo hayo ni moja ya juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuhakikisha kuwa elimu kuhusu udhibiti wa vifaa vya kemikali inaendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali katika jamii.

“Tumepanga mafunzo haya pia yatolewe kwa upande wa Zanzibar kwa kuwa kule kuna bandari ambayo inatumika kuingiza na kupokea bidhaa za aina mbalimbali ikiwemo kemikali….Tumekusudia mafunzo haya kuwa endelevu ili tuweze kujenga uelewa wa pamoja kwa jamii” amesema Kemilembe.

Naye Afisa Ununuzi na Ugavi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Stanslaus Kagali ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuandaa mafunzo hayo yamewapa uelewa kuhusu umuhimu wa ukomo wa matumizi ya vifaa vyenye kemikali ikiwemo majokofu na ambavyo mara kwa mara vimekuwa vikinunuliwa na Serikali.

“Asilimia 75 ya fedha za Serikali zinahusiana na huduma za ununuzi na ugavi...Tunashukuru kupatiwa mafunzo haya kwa kuwa yanatuwezesha kubaini aina ya vifaa ambavyo havifai kwa ajili ya matumizi kutokana na madhara yake kwa afya ya binadamu na mazingira” amesema Kagali.

Mafunzo hayo ya siku mbili yashirikisha jumla ya maafisa ununuzi kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na Watoa mada kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA).

Settings