Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, 2024 Bw. Godfrey Mnzava amesema mtu anapoomba kibali cha ujenzi wa makazi lazima aelekezwe moja ya sharti ni kupanda miti angalau mitano, mitatu ikiwa ya matunda na miwili ya kivuli.
Bw. Mnzava amesema hayo Aprili 4,2024 katika Uwanja wa CCM Sanya Juu Halmashauri ya Siha mkoani Kilimanjaro alipokuwa akiongea na wananchi juu ya madhara ya uharibifu wa Mazingira akisema Mazingira ukiyaadhibu hayachukui muda mrefu nayo yanakuadhibu.
Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Siha imekuwa ikikusanya taka tani 90 hadi 100 kwa mwezi ikiwa moja ya njia ya kuweka mji safi kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Mazingira ya wilaya hiyo.
Imeeleza pamoja na mafanikio ya ukusanyaji wa taka bado halmashauri inakumbwa na changamoto ya kutokuwa na dampo la kisasa. Wilaya ya Siha imekuwa ikidhibiti taka ngumu kwa kutumia magulio sita ambayo ni Sanya Juu, Lawate, Ngarenairobi, Makiwaru, Karansi na Kidire ambayo hutumika katika ukusanyaji wa taka.
“Makadilio ya taka zinazokusanywa kwa mwezi katika magulio hayo hufikia tani 90 hadi 100 kulingana na mazingira ya magulio ya siku husika na hali ya usafi imekuwa ikiendelea kuimarika.
“Utaratibu unaotumika ni kwa kuunda Umoja wa Wafanyabiashara katika magulio hayo ambapo wanachangia gharama za usafi kuanzia shilingi 200 hadi 300 na usafi hufanyika kila baada ya kufanyika gulio,” ilieleza taarifa hiyo.
Hata hivyo bado kumekuwa na changamoto ya kutokuwepo kwa dampo ya kisasa kwa ajili ya kuhifadhia taka, kwani taka zinazokusanywa hutupwa kwenye mashimo ya machimbo ya mchanga.
Kwa upande wa upandaji wa miti iliyooteshwa mwaka huu hadi kufikia Machi 30,2024 ilikuwa 952,000 huku siku ya kukimbiza Mwenge wa Uhuru katika Shule ya Kata ya Ormelili ikipandwa miti 10 sawa na miti iliyopandwa katika Shule Msingi Sanya Juu.
Taarifa za miti iliyopandwa kwa mwaka 2022/23 Halmashauri ya Wilaya ya Siha ilikuwa 1,214,650 huku miti iliyopandwa siku saba wakati wa kukimbiza Mwenge wa Uhuru ikiwa 1,534. “Miti 992 ilipandwa wakati wa ufunguzi wa Shule ya Awali na Msingi Munge, Ufunguzi wa madarasa na Ofisi ya Shule ya Msingi ya Kishisha 286, Shamba la mwekezaji Macademia ikipandwa 30.
“Barabara ya Sanya Juu – Naibili hadi KIA ikipandwa miti 10, Zahanati ya Baibili ikipandwa miti 156, mradi wa Maji Gararagua – Ndinyika ikipandwa miti 60 na Shule ya Sekondari Skirali ikipandwa miti 10.”
Mkuu wa Wilaya laya ya Siha, Christopher Timbuka amesema kati ya miti 1,214,650 iliyopandwa mwaka jana miti ilikua vizuri hadi sasa ni miti 868. Timbuka ameongeza kuwa wataendela kutunza mazingira kwa kuhakikisha miti iliyopandwa inalindwa na kutunza vizuri ili iweze kukua kama lengo lililokusudiwa na serikali.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2024 inasema “ Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”.