​Wananchi watakiwa kuacha kuharibu kingo za mito

May, 07 2021

Serikali imewataka wananchi kuacha shughuli zinazosababisha uharibifu wa kingo za mito huo na badala yake wapande miti na majani yanayozuia ubomokaji wa kingo hizo.

Hayo yamesemwa leo Mei 7, 2021 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande wakati akijibu swali la Mbunge wa Mpwapwa, Mhe. George Natany Malima aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kutengeneza kingo za korongo linalopita katikati ya Mji wa Mpwapwa mkoani Dodoma lisiendelee kutanuka ili kunusuru maisha na makazi ya wananchi wa maeneo hayo.

Katika majibu yake Mhe. Chande alisema ili kukabiliana na athari zinazotokana na uharibifu huo wa mazingira, Serikali imefanya upembuzi wa awali kwenye mto kiasi cha urefu upatao km. 2 ambazo ziko jirani na makazi ya watu ili kufahamu gharama za kudhibiti kingo zake.

Alisema katika upembuzi huo inakadiriwa kwamba zinahitajika sh. bilioni 2.17 ambazo zitatumika kwa ajili ya kuweka gabioni mita za ujazo 8,870, kujenga vizuri mmomonyoko kwa zege mita za ujazo 52 na kujaza udongo maeneo yote yaliyobomoka kiasi cha mita za ujazo 9,000.

Aidha, Chande aliongeza kuwa pia kazi nyingine inayotarajiwa kufanywa ni kurudisha mto kwenye mkondo wake wa asili ambapo kinahitajika kifusi kiasi cha meta za ujazo 6,000 hivyo Serikali imetenga fedha ili kuweza kutekeleza mradi huu.

“Mji wa Mpwapwa umejengwa pembezoni mwa Mto ambao ni maarufu kwa jina la Mto Shaban Robert ambao sasa unaonekana kama korongo linalopita katikati ya Mji. Kutokana na wananchi kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwenye kingo za Mto huo, kumekuwa na kubomoka kwa kingo zake. Hali hii imeleta athari kubwa kwenye miundombinu na makazi ya watu walioko karibu na kingo za mto huo,” alisema.

Settings