Wananchi wasifanye shughuli kwenye fukwe

Nov, 07 2023

Serikali imewataka wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya eneo la mita 60 katika kingo za mito, fukwe za bahari na maziwa ili kuepusha uharibifu wa mazingira.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis bungeni leo Novemba 7, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Kawe Mhe. Askofu Josephat Gwajima aliyetaka kujua mipango wa Serikali kudhibiti Mto Nakasangwe na Tegeta inayopanuka kwa kasi na kutishia maisha ya watu na mali.

Mhe. Khamis amesisitiza utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 kuhusu Hifadhi ya Eneo la Mita 60 kutoka vyanzo hivyo vya maji inayozuia matumizi yoyote ya kibinadamu katika maeneo hayo.

Amesema kwa kutambua kupanuka kwa kingo za mito hiyo iliyopo mkoani Dar es Salaam, Naibu Waziri amesema Serikali itaangalia uwezekano wa kufanya tathmini katika maeneo mengine ambapo ilibuni na kutekeleza miradi ya ujenzi wa kuta kama vile Pangani na fukwe katika Barabara ya Barack Obama jijini humo.

Akiendelea kujibu swali hilo, amefafanua kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto za kupanuka kwa mito hiyo zikiwemo kuandaa Mwongozo wa Usafishaji Mchanga, Tope na Taka ngumu kwenye mito na mabonde Dar es Salaam.

“Ili kukabiliana na changamoto hizi tumeendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa vyanzo vya maji katika ngazi zote ili kuongezeka kasi ya hifadhi vya maji na kingo za mito, pia kuhamasisha upandaji wa miti rafiki kwa vyanzo vya maji ambayo itasaidia katika kuzuia mmomonyoko wa kingo za mito na kuimarisha mtiririko wa maji,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mhe. Khamis amesema Serikali inatarajia kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu itakayosaidia katika kutatua changamoto ya mafuriko yanayotokea wakati wa msimu wa mvua katika maeneo mbalimbali nchini.

Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Gwajima kuhusu mpango wa dharula wa Serikali wa kukabiliana na athari za mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, ameongeza kuwa elimu itaendelea kuwahimiza wananchi waondoke kwenye maeneo yasiyo salama.

Settings