Wananchi wahimizwa kulinda miti inayopandwa

Jan, 27 2024

Wananchi wametakiwa kuitunza na kuilinda miti inayopandwa katika maeneo mbalimbali ili iweze kukua hivyo kuleta faida kwa jamii na kufikia malengo ya kukihifadhi mazingira.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dkt. Khamis Mkanachi ambaye alimwakilishi Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda katika zoezi la upandaji miti eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuelekea Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano.

Dkt. Mkanachi amesema kuwa jukumu la kulinda miti hiyo si tu la viongozi wa chuo hicho bali linatakiwa litekelezwe pia na viongozi wa Serikali ya Mtaa.

Amesema ni matarajio kuwa zoezi hilo liwe endelevu na kupata matokeo chanya yakiwemo halmashauri zote nane za Mkoa wa Dodoma zikipanda miti 1,500,000 kwa mwaka, lengo la kupanda miti Milioni 40 kufikia mwaka 2025 litafikiwa.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema zoezi la upandaji miti linaloendelea mkoani Dodoma ni uungwaji mkono kampeni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyoizundua mwaka 2017 akiwa Makamu wa Rais.

“Sote tutakumbuka Desemba 5, 2017 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua rasmi Kampeni ya Kukijanisha Dodoma hivyo tukipanda miti inakuwa sehemu ya kuunga mkono jitihada zake ambaye hivi sasa ndiye Rais wetu.

Bw. Mitawi amesema tunapanda miti kuelekea kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiwa ni jitihada za waasisi wetu pamoja na kuunga mkono jitihada na mchango za wakuu wetu katika kupanda miti na kukijanisha Dodoma.

“Nimefarajika kuona wengi waliokuwepo hapa ni vijana ambao ndio wanapanda miti, hivyo lazima tujivunie katika hilo na hii ndio inaonyesha wajibu wetu kwa jamii,” amesema Mitawi.

Ameongeza mti unaopandwa leo ndio maisha ya watu ya baadaye, hewa itakayotumika kesho itakuwa imechangiwa na miti ambayo inapandwa sasa, hivyo hata miti itakayopandwa natumai itakuwa tofauti sababu inapandwa na wasomi.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka amesema lengo la chuo hicho kwa mwaka huu kupanda miti 30,000 hivyo wanaimani siku za mbele watu watakwenda kujifunza juu ya jambo hilo wanalolifanya kwa sasa.

Settings