Wananachi watakiwa kuitunza miradi ili iendelee kuwanufaisha

Mar, 09 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe Harusi Said Suleiman amewataka wananchi kuitunza miradi inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao ili waendelee kunuifaika nayo.

Ametoa witoa huo wakati wa ziara ya Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi katika Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Machi 09, 2024.

Mhe. Harus amewaomba wananchi wa eneo hilo kuilinda miradi hiyo kwani itawaletea faida kubwa ikiwemo kupata ajira zitakazowaongezea kipato na hivyo kuongeza uchumi.

Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Mvomero Bw. Said Nguya amesema mradi huo umewezesha ujenzi wa lambo moja kwa ajili ya kueneza teknolojia ya uvunaji wa maji, ujenzi wa kiwanda cha kuchakata bidhaa za ngozi, uzalishaji wa samaki na ujenzi wa jengo la kukusanyia maziwa.

Mratibu wa Mradi huo Kitaifa, Dkt. Makuru Nyarobi amesema lengo la Mradi wa EBARR ni kuwajengea uwezo wananchi katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya Tabianchi kwa kuwapatia mbinu na teknolojia za kiikolojia katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Mradi huu umejenga lambo lenye upana wa mita 20 na kimo cha mita saba ikiwa na uwezo wa kukusanya maji lita za ujazo zaidi ya laki mbili zinazoweza kumwagilia hekta 287 ambapo maji haya huwasaidia pia wananchi wa Kijiji cha Melela kukabiliana na changamoto ya uhaba wa maji,” amesema Dkt. Nyarobi.

Mradi wa EBARR unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais pia umesaidia kuwezesha wananchi kiuchumi kwa kuanzisha kilimo cha uyoga kama njia mbadala ya kujiongezea kipato na kuimarisha lishe.

Shughuli za mradi ni zinatekelezwa katika ngazi za vijiji ili kuwajengea wananchi uelewa na utayari wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Settings