Wadau wa sekta watakiwa kuongeza nguvu kukabili mabadiliko ya tabianchi

Oct, 24 2023

Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Bi. Farhat Mbarouk ametoa wito kwa wadau kutoka sekta mbalimbali wametakiwa kuongeza nguvu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayokabili Tanzania.

Ametoa wito huo wakati akifunga Warsha ya Wadau wa Kitaifa kuhusu maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP28.

Warsha hiyo imefanyika kuanzia Oktoba 23 hadi 25, 2023 jijini Arusha na kushirikisha Wizara, Taasisi za Serikali na Binafsi, Sekta Binafsi, Mashirika ya Kimataifa, Ofisi za Balozi zilizopo nchini na Asasi za Kiraia kuhusu fursa mbalimbali za fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinazotolewa na Mifuko ya Kimataifa na nchi mbalimbali duniani.

Bi. Farhat amesema kuwa mabadiliko ya tabianchi hayana mipaka, hivyo ni lazima wadau wote wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja na si kila mmoja kwa wakati wake.

Amesema mawasilisho yaliyotolewa na kujadiliwa katika warsha hiyo yameweka msingi imara kwa Tanzania kushiriki ipasavyo katika COP28 inayokuja nchini na kwamba kupitia tathmini malengo yote muhimu yametimizwa kikamilifu.

“Kwa niaba ya Ofisi ya Makamu wa Rais natoa shukrani zangu za dhati kwenu nyote kwa ushiriki wenu katika warsha hii ya Wadau wa Kitaifa kuhusu maandalizi ya ushiriki wa Mkutano wa COP28,” amesema.

Aidha, Mkurugenzi Farhat amewashukuru wadau kutoka Benki ya Dunia na Maendeleo ya Nchi za Nje na Jumuiya ya Madola ambao wamefanikisha warsha hiyo kwa mafanikio.

Warsha hiyo imefanyika jijini Arusha Oktoba 24, 2023 kwa lengo la kujenga uelewa kwa washiriki kuhusu fursa mbalimbali za fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinazotolewa na Mifuko ya Kimataifa na nchi mbalimbali duniani.

Mkutano wa COP28 unatarajiwa kufanyika Dubai, Muungano wa Falme kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023 ukichagizwa na Kaulimbiu ya kitaifa “Kuimarisha Kilimo Himilivu na Uchumi wa Bluu katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi”.

Settings