Serikali ya Tanzania imeikumbusha Jumuiya ya Kimataifa hususan nchi zilizoendelea kutekeleza jukumu lake na kuwezesha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa Mkakati wa Dunia wa kuhifadhi Bioanuai kuendana na ibara ya 20 na 21 ya Mkataba wa Bioanui.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema hayo Oktoba 29, 2024 alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa 16 wa Wakuu wa Nchi wa Uhifadhi wa Mazingira unaofanyika jijini Cali, Colombia.
Sanjari na hilo, Mhe.Dkt. Kijaji amewakumbusha wadau kutoka nchi zinazoendelea kuwekeza rasilimali zitakazowezesha utekelezaji wa mikakati hiyo kuwezesha fedha za kuhifadhi bionauai katika nchi zinazoendelea.
Akiendelea kuzungumza wakati wa mkutano huo, amesema kuwa Tanzania tayari imekwishatenga eneo la ardhi la zaidi ya asilimia 40 kwa ajili ya hifadhi ya bioanuai.
Sanjari na hatua hiyo pia, Mhe. Dkt. Kijaji ameelezea namna Serikali ya Tanzania inavyofanya maboresho makubwa katika taasisi za masuala ya uhifadhi nchini, mapitio ya nyenzo za kisera za masuala ya uhifadhi wa bioanuai na mazingira.
Ameongeza kuwa Tanzania ipo katika hatua za kufanya mapitio ya Mkakati wa Taifa wa Kuhifadhi Bioanuai nchini, ambapo utekelezaji wa Mkakati huo ni mchango wa kitaifa katika kufikiwa kwa dhima ya kidunia ya kuwa na mazingira bora Duniani ifikapo mwaka 2050.
Mkutano wa 16 wa Wakuu wa Nchi wa Uhifadhi wa Mazingira ulifunguliwa Oktoba 21, 2024 na utarajiwa kufungwa malizika Novemba mosi, 2024.