Tanzania yapunguza asilimia 86 ya kemikali hatarishi kwa Tabaka la Ozoni

Sep, 16 2020

Tanzania imepunguza zaidi ya tani 216 sawa na asilimia 86 ya kiasi cha matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni azma ikiwa ni kuondosha matumizi ya kemikali hizi kufikia mwaka 2030.

Haya yamesemwa hii leo Jijini Dodoma na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuadhimishia Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni kupitia Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene.

Alisema, katika jitihada za kuhifadhi Tabaka la Ozoni, mwaka 1996, Serikali ya Tanzania iliandaa na kutekeleza Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni ili kuhakikisha kwamba hakuna sekta ya uchumi au jamii inaathirika kutokana na matakwa ya Itifaki ya Montreal. Aidha, programu hii ilianzisha utaratibu wa kusimamia na kudhibiti uingizaji wa kemikali na bidhaa zenye kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni kutoka nje ya nchi.

Kwa upande mwingine Mheshimiwa Makamu wa Rais aliikumbusha jamii wajibu wa kuendelea kulinda tabaka la ozoni kwa kuepuka kuingiza nchini kemikali na vifaa vinavyotumika kumong’onyoa tabaka la ozoni kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika (mtumba) bali kuingiza nchini vipoozi mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni.

“Natoa rai kwa jamii kununua bidhaa zilizowekwa nembo ya “Ozone friendly” yaani ‘sahibu wa Ozoni’ au “CFC-free” ikiashiria haina wala haikutengenezwa na kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni, kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani ama vifaa vya kuzima moto vyenye kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni” Alisisitiza Makamu wa Rais.

Maadhimisho ya mwaka huu yalienda sambamba na utoaji wa zawadi kwa washindi wa insha kuhusu mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya bioanuai kwa ngazi za Shule ya Msingi, Sekondari na Vyuo vya Elimu ya Juu kwa lengo la kukuza na kupima uelewa, kuhamasisha ubunifu kwa wanafunzi na vijana kuhusu mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya bioanuai.

Pia alitoa wito kwa washirika wa maendeleo kuunga mkono jitihada za kutunza mazingira katika: kuhifadhi tabaka la ozoni; kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi; kuhifadhi bioanuai na usafi wa mazingira. Pia, kuhusisha vijana wadogo na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za mazingira ili kuwa na kizazi chenye uelewa na kinachothamini hifadhi ya mazingira.

Awali, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine alisema juhudi za kulinda Tabaka la Ozoni zinaendelea kupata mafanikio duniani na kusisitiza kuwa huenda litarejea katika hali yake ya awali takribani miaka 30 mpaka 50 ijayo endapo hapatakuwa na kemikali haribifu zitakazoingia tena angani. “Juhudi zozote za kupunguza matumizi ya kemikali hizo zitaleta matokeo ya manufaa kwenye kurejesha tabaka la Ozoni katika hali ya kawaida. Juhudi za kila mmoja wetu zinatakiwa ili kupunguza na kuondosha madhara katika Tabaka la Ozoni yanayosababishwa na shughuli zetu tunazofanya” alisisitiza Balozi Sokoine.

Ozoni ni tabaka la hewa lililopo kwenye angahewa ya juu, takribani kilometa 15 hadi 30 juu ya ardhi likiwa na kazi ya kuchuja kiwango kikubwa cha mionzi ya jua isifike kwenye uso wa dunia. Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya ni “Miaka 35 ya Kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa manufaa ya afya ya binadamu na mazingira” (Ozone for Life35 years of Ozone Layer Protection). Kaulimbiu hii inatukumbusha umuhimu wa kulinda na kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa kupunguza uzalishaji na matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa Tabaka hili.

Settings