Tanzania inatarajia kushiriki na kuongoza ushiriki wa nchi za Afrika katika Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) utakaofanyika jijini Belem, nchini Brazil, kuanzia Novemba 10 hadi 21, 2025 ambapo Ujumbe wa Tanzania unatarajiwa kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Maandalizi ya Kitaifa ya Msimamo wa Taifa Kuelekea Ushiriki wa Nchi katika mkutano wa COP 30 uliofanyika jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 6, 2025.
Mhandisi Luhemeja amesema kuwa Tanzania kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kundi la Nchi za Afrika la Watalaamu wa Mabadiliko ya Tabianchi (Africa Group of Negotiators – AGN) hivyo, inatarajiwa kuongoza majadiliano na kuzungumza kwa niaba ya bara la Afrika katika mijadala inayohusu mabadiliko ya tabianchi yatakayofanyika wakati wa COP30.
Katika mkutano huo Tanzania inatarajia kubeba vipaumbele vya kitaifa na bara la Afrika katika suluhisho la changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Hivyo, kwa Tanzania, huu si mkutano wa mazungumzo tu bali unahusu kuanzisha ubia na kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali ya kutosheleza kwa ajili ya kulinda watu wetu, mifumo ikolojia na uchumi stahimilivu kutokana na athari zinazoongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza, Mkurugenzi Mtendaji wa CAN Tanzania Dkt. Sixbert Mwanga amesema kuwepo kwa kikao hicho kitasaidia kuwaandaa wadau wote kuwa na kauli moja na kuifanya Tanzania kupata kile kilichokusudia katika COP30. Baada ya kushiriki kwa mafanikio katika COP29 huko Baku, Azerbaijan, mwaka jana, COP30 ni wakati wa kihistoria kwa ajenda ya kimataifa ya hali ya hewa. Mkutano wa 30 unatarajiwa kufafanua ramani ya barabara na hatua za haraka katika kukusanya fedha kiasi cha Dola za Marekani 1.3 Bilioni zinazohitajika kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani.